1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazoezi makubwa ya kijeshi ya NATO yaanza Norway

25 Oktoba 2018

Jumuiya ya kujihami NATO imeanza zoezi kubwa la kijeshi tangu enzi ya vita baridi. Zoezi hilo linalofanyika nchini Norway ni la majaribio ya kujibu mashambulizi iwapo mwanachama mmoja wa Jumuiya hiyo atashambuliwa.

Norwegen Nato-Großmanöver «Trident Juncture»
Picha: picture-alliance/dpa/M. Assanimoghaddam

Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo ya kujihami NATO Jens Stoltenberg amesema watafanya majaribio ya uwezekano wa kujibu changamoto za kiusalama, zinazosababishwa na Urusi tangu mwaka 2014, kufuatia nchi hiyo kuitwaa kimabavu rasi ya Crimea na pia hatua zake zinazoonekana kama jitihada za kuyumbisha usalama wa mataifa ya Magharibi.

Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo ya kujihami NATO Jens StoltenbergPicha: picture-alliance/dpa/F. Seco

Wanachana wote 29 wa NATO pamoja na nchi washirika Sweden na Finland watashiriki katika mazoezi hayo ya ardhini, majini angani na mitandaoni yanayoanza leo hadi tarehe 7 Novemba.

Kulingana na msemaji wa kijeshi wa Norway Ivar Moen tayari vikosi vyote vimekwishawasili na viko katika maeneo yao.

Zoezi hilo litawajumuisha wanajeshi 50,000, magari ya kijeshi 10,000 na zaidi ya ndege za kivita na meli 300 ili kulinda nchi wanachama kutokana na mashambulizi.

Nchi tano kubwa zinazochangia majeshi yake ni Marekani, Ujerumani, Norway, Uingereza na Sweden.

Urusi imekasirishwa na mazoezi ya kijeshi ya Jumuiya ya kujihami NATO

Urusi kwa upande wake imealikwa kutuma waangalizi nchini Norway, hatua ambayo Stoltenberg ameisifu akiitaja kuwa ya wazi.

Amesema iwapo Urusi itashiriki kwa heshima na kujiepusha na hatari yoyote haoni sababu ya taifa hilo kutoalikwa kufuatilia mazoezi hayo yanavyokwenda.

Rais wa Urusi Vladimir Putina na Waziri wake wa Ulinzi Sergei ShoiguPicha: Imago/ITAR-TASS/M. Klimentyev

Hata hivyo Uruisi imekasirishwa na zoezi hilo huku Waziri wa wake wa ulinzi akionya kwamba huenda wakalazimika  kujibu kufuatia shughuli zaidi zinazofanyika karibu na mpaka wake eneo la Magharibi.

Mapema mwaka huu Urusi iliandaa zoezi kubwa kabisa la kijeshi mashariki mwa nchi hiyo lililopewa jina la vostok.

Urusi inasema zaidi ya wanajeshi 300,000 walishiriki zoezi hilo lakini wanadiplomasia wa Magharibi wanasema idadi hiyo imeongezwa.

Mwandishi:  Amina AbubakarIAFP/AP/dpa

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW