Mazungumzo ya DRC na waasi wa M23 yaripotiwa kwenda vizuri
11 Julai 2025
Juma lililopita Waasi wa Kundi la M23 walitoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo zaidi ili kushughulikia matatizo ambayo hayakujumuishwa katika makubaliano ya amani kati ya Kigali na Kinshasa yaliyotiwa saini mjini Washington mwezi Juni, kwa lengo la kumaliza mapigano ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu mashariki mwa Kongo.
Habari ya mafanikio hatua hii ya sasa imetolewa na mwanadiplomasia wa Qatar kwa sharti la kutotajwa jina lake akisisitiza kuwa wawakilishi wa pande hizo mbili wanajadiliana kuhusu namna ya kupunguza mateso ya wakazi wa Mashariki mwa Kongo, kuimarisha mpango wa usitishaji mapigano na kuhimiza hatua zaidi kuelekea maridhiano.
Kundi la M23 linasema muhimu kwa sasa ni kujenga hali ya kuaminiana
DW imefanikiwa kumpata msemaji wa kundi hilo, Lawrence Kanyuka akiwa mjini Goma ambae alitoa dokezo ya yale muhumu ambayo yanatokea sasa mjini Doha akisema "Kimsingi, kile tunachosema kwa kinachotekea Doha, tupo katika hatua ambapo pande zote tunaziwasilisha mezani na kuonesha hatua zitakazokuwa katika msingi wa kuaminiania. Kwa hivyo kujenga uaminifu, kabla hatujaendelea na mazungumzo, tunapaswa kuwa katika mazingira ya kuaminiana."
Msemaji huo wa M23 aliongeza kwa kusema "Serikali ya Kinshasa kwa mfano, imeainisha mambo kadhaa ambayo inataka sisi tuyaheshimu. Kwa upande wetu tumeiomba Kinshasa vitu vya msingi. Tumewaomba kuwaachilia huru wafungwa wetu, kama tulivyofanya kuwachia wafungwa wote wa jeshi la Kongo na wapiganaji Wazalendo waliokuwepo mjini Goma katika eneo la Monusco, tukawapeleka mpakani na wakaenda Kinshasa."
Msingi wa makubaliano kati ya DRC na Rwanda
Kimsingi makubaliano yaliyosainiwa kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda yalilenga kumaliza mapigano ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu katika eneo la mashariki mwa Kongo lenye utajiri wa madini.
Hata hivyo, kundi la waasi la M23, ambalo ndilo kundi kubwa linalopigana na majeshi ya serikali ya Kongo, halikuhudhuria mazungumzo ya Washington na liktaoa wito wa kufikiwa kwa makubaliano tofauti ya kusitisha mapigano na serikali ya DRC.
Kundi hilo limeyateka maeneo makubwa ya mashariki mwa Kongo katika mashambulizi ya kushtukiza ya mwezi Januari na Februari, ikiwa ni pamoja na miji ya kimkakati ya mikoa ya Goma na Bukavu.
Mgogoro umelikumba eneo hilo kwa zaidi ya miongo mitatu, na kusababisha mamia ya maelfu ya watu kuyakimbia makazi yao.
Rwanda, ambayo ni jirani na DRC, inakanusha kutoa msaada wa kijeshi kwa kundi la M23, lakini wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa jeshi la Rwanda limekuwa na mchango "muhimu” katika mashambulizi ya M23 ikiwa ni pamoja na kushiriki moja kwa moja katika mapigano.