1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani kati ya Urusi na Ukraine yaahirishwa

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
14 Machi 2022

Duru ya nne ya mazungumzo kati ya Urusi na Ukraineyaliyokuwa yanafanyika kwa njia ya video imeahirishwa hadi kesho Jumanne. Lakini mapambano makali bado yanaendelea na watu kadhaa wameuawa katika pande zote mbili.

Ukraine | Zerstörte Gebäude in Kharkiv
Picha: Sergey Bobok/AFP/Getty Images

Mshauri wa Rais wa Ukraine Mykhailo Podolyak, amesema duru ya nne ya mazungumzo hayo imeahirishwa hadi hapo kesho. Podolyak ambaye ni mpatanishi anayeiwakilisha serikali ya Ukraine amesema hatua hiyo imechukuliwa ili kamati za kiufundi za pande zote zishughulikie ufafanuzi zaidi wa masuala mabalimbali katika mazungumzo hayo. Ukraine imesema mazungumzo hayo magumu yanalenga kusitisha mapigano licha ya jengo la makazi ya watu katika mji wake mkuu Kyiv kushambuliwa.

Wajumbe wa Urusi na Ukraine katika mazungumzo ya kusiamisha mapigano Picha: Sergei Kholodilin/BELTA/AFP

Wakati huo huo, shirika la habari la Associated Press (AP) limeripoti juu ya kuuawa mwanamke mjamzito baada ya majeshi ya Urusi kuilipua hospitali ya wazazi ambako mwanamke huyo alikusudiwa kujifungua.

Kwa upande wake jeshi la Urusi limesema raia 20 ni miongoni mwa watu waliouawa katika shambulio la kombora la masafa marefu lililorushwa na vikosi vya Ukraine. Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi Meja Jenerali Igor Konashenkov amesema kombora aina ya Tochka-U lilipiga sehemu ya kati ya mji wa mashariki wa Donetsk. Amesema raia wengine 28 wakiwemo watoto wamejeruhiwa vibaya. Konashenkov amesema kombora hilo lilirushwa kutoka eneo la kaskazini magharibi mwa mkoa wa Donetsk unaodhibitiwa na vikosi vya Ukraine.

Umoja wa Mataifa umesema takriban wati 636 wameuawa katika vita vya Ukraine. Kulingana na mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi Filippo Grandi, wakimbizi wanaokimbia Ukraine wamefikia karibu milioni 2.7. Amesema huu ni msafara mkubwa zaidi wa wakimbizi barani Ulaya tangu Vita vya Pili vya Dunia.

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR Filippo Grandi.Picha: Lev Radin/Pacific Press/picture alliance

Nayo kampuni ya nishati ya Ukraine imesema njia ya kupelekea nishati kwenye kinu cha nyuklia kilichopatwa na maafa imeharibiwa tena na majeshi ya Urusi baada ya kutengenezwa hapo awali. Kampuni hiyo Ukrenergo imeeleza katika tamko leo kuwa mafundi wake walianza ugavi wa nishati hapo jana lakini kabla ya nishati kurejeshwa kikamilifu majeshi ya Urusi yanayoikalia sehemu hiyo yalikiharibu tena. Hata hivyo kampuni hiyo imesema itajaribu kukitengeneza tena. Nishati hiyo inatumika kwa ajili ya kujaza mabomba na vifaa vingine vinavopooza nishati ya nyukulia iliyotumika kwenye kiwanda hicho cha nyuklia cha zamani na pia kuzuia uvujaji wa miali.

Kiwanda cha nyuklia cha zamani cha ChernobylPicha: STR/NUR Photo/picture alliance

Hata hivyo, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki limeondoa wasiwasi juu ya usalama wa taka za nyuklia katika kinu cha Chernobyl, limesema mabwawa ya kupoza ni makubwa na yana nafasi ya kutosha ya kuhifadhi mafuta yaliyotumika katika viwango salama hata kama umeme utakuwa umekatizwa.

Vyanzo:RTRE/AP