1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo kuhusu Iran yaingia duru muhimu

9 Novemba 2013

Mazungumzo kati ya Iran na nchi zenye nguvu zaidi duniani yanaingia siku ya tatu huku wanadiplomasia wanaotafuta ufumbuzi wa mzozo kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran wakionya kuwa vikwazo vikubwa bado vipo.

Picha: Reuters

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry aliyesitisha ziara yake Mashariki ya kati kuhudhuria mazungumzo hayo kuhusu Iran yanayofanyika mjini Geneva Uswizi, ameonya kuwa bado hakuna maafikiano kwani kuna masuala muhimu sana mezani ambayo bado hayajatatuliwa.

Kerry amejiunga na mawaziri wenzake wa mambo ya nje kutoka Ujerumani,Ufaransa na Uingereza, na matumaini yanaongezeka hasa baada ya taarifa kuwa waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov anatarajiwa kuhudhuria leo.

Kuwasili kwa Lavrov kutawaleta pamoja mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zote wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ambao kwa muongo mmoja wamekuwa wakiujadili mpango wa utatanishi wa kinyuklia wa Iran.

Bado hakujaafikiwa makubaliano

Hapo jana, Kerry,mwenzake wa Iran Javad Zarif na mkuu wa sera za kigeni wa umoja wa Ulaya Bi Catherine Ashton anayeziwakilisha nchi sita zenye nguvu zaidi duniani katika mazungumzo hayo walikutana hadi usiku.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad ZarifPicha: Reuters

Mkutano huo uliishia kwa Kerry kusema kuwa bado kuna kazi kubwa inayowakabili kabla ya kuafikiana.Mkutano huo unatarajiwa kuendelea leo asubuhi.

Ikiwa makubaliano yatafikiwa ,basi hatua hiyo itakuwa ya kuuondoa mkwamo ambao umekuweko kwa muongo mzima kati ya Iran na nchi hizo sita zinazojumuisha Ufaransa,Uingereza,Urusi,China,Marekani na Ujerumani.

Makubaliano yanayotarajiwa, yanayozingatiwa kuwa hatua ya kwanza ya kulifikia suluhisho, yatakuwa na maana ya Iran kuzisimamisha shughuli zake za kinyukilia kwa muda wa miezi sita ,ili vikwazo vilivyoubana uchumi wa nchi hiyo vilegezwe.

Ripoti zinaarifu kuwa makubaliano yanayopendekezwa huenda yakawa na maana ya Iran kuacha kuyarutubisha madini ya urania kwa asilimia 20.

Je Iran itakubali kusitisha mpango wa kinyuklia?

Kiwango hicho ni hatua chache tu kufikia uwezo wa kuunda silaha za nyuklia.Kwa mujibu wa mapendekezo yanayotarajiwa Iran pia itapunguza milundiko ya madini ya urania na kukubali kuacha kukifanyisha kazi kinu chake cha plutonium cha Arak.

Lakini mapendekezo hayo yamepingwa vikali na Israel.Waziri mkuu wake Benjamin Netanyahu ameitaka jumuiya ya kimataifa kutozingatia kulegeza vikwazo dhidi ya Iran kwani anahoji ,kufanya hivyo ni kuinufaisha Iran na jumuiya ya kimataifa itakuwa imepoteza.

John Kerry na Waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Reuters

Marekani imezipinga shutuma hizo za Israel kupitia msemaji wa ikulu Josh Earnest aliyesema bado hakuna maafikiano yoyote na ameeleza kuwa kwa sasa kutoa shutuma ni mapema mno.Taarifa kutoka ikulu hiyo imesema Rais Barrack Obama alimpigia simu Netanyahu kutokana na matamshi yake.

Iran imekuwa ikikanusha mara kwa mara madai kuwa mpango wake huo wa kinyuklia ni kwa minajili ya kuunda silaha. Wakati wote imekuwa inasisittiza kuwa mpango wake ni wa amani na wa matumzi ya nishati ya nchi yake.

Tangu kuingia madarakani kwa Rais Hassan Rouhani mwaka huu,hatua muhimu zimepigwa katika kutafuta ufumbuzi wa mzozo huo wa muda mrefu.

Iran inakusudia kuuboresha uchumi wake hasa kwa mapato yatokanayo na uuzaji wa mafuta yake ambao kwa sasa umekwamishwa na vikwazo vilivyowekwa hasa na nchi za magharibi.

Nazo nchi za magharibi zinatumai kuchukua fursa hiyo ya nadra kuboresha uhusiano wa kidiplomasia na Iran ili pia kufungua milango ya majadiliano ya masuala mengine muhimu kama mzozo wa nchi jirani Syria ambako Iran imekuwa ikimuunga mkono Rais Bashar al Assad dhidi ya waasi wanaotaka kumng'oa madarakani.

Mwandishi:Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Mtullya Abdu