Mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yapiga hatua
9 Aprili 2014Abbas Araqchi amesema pande zote mbili katika mazungumzo hayo zimepunguza tofauti kubwa zilizokuwepo na kuongeza kuwa mazungumzo hayo yanayonuia kuumaliza mzozo wa muda mrefu bado ni magumu.
Duru hii ya hivi punde ya mazungumzo ya kuelekea kutafuta makubaliano kamili kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran yalianza hapo jana mjini Vienna na yanatarajiwa kukamilika baadaye hii leo.
Bado kazi kubwa ipo
Katika taarifa ya pamoja,Waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton wamesema kazi kabambe bado inahitajika kuweza kumaliza tofauti zilizopo kati ya pande zote mbili.
Afisa mwandamizi wa serikali ya Marekani anayehusika katika mazungumzo hayo amesema mazungumzo hayo yanayoendelea Vienna,Austria, yanajaribu kupiga hatua za kuridhisha kuwezesha kuanza kuandikwa kwa mkataba wa makubaliano kamili tarehe 13 mwezi ujao ambapo duru nyingine inatarajiwa kufanyika.
Iran inatarajiwa na nchi wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani kuusitisha kabisa mpango wake wa kinyuklia ili kutuliza hofu kuwa ina dhamira ya kuunda zana za kinyuklia, madai ambayo Iran imekanusha mara kwa mara.
Siku ya Jumatatu waziri wa mambo ya nje wa Marekani Joh Kerry aliwaambia wabunge wa nchi yake kimsingi Iran inaweza kuunda bomu la kinyuklia iwapo ikiamua kufanya hivyo katika kipindi cha miezi miwili.
Makubaliano kamili yatarajiwa Mei
Mwezi Novemba mwaka jana, Iran ilikubaliana na nchi hizo zenye nguvu kupunguza urutubishaji wake wa madini ya Urani kwa kiwango kinachokubaliwa na shirika la kimataifa la kudhibiti nishati ya Atomiki IAEA.
Makubaliano hayo ya Novemba hata hivyo yalikuwa ya muda tu na pande hizo mbili zinatarajiwa kufikia makubaliano kamili kabla ya tarehe 20 mwezi Julai.
Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amenukuliwa hii leo akisema Iran inapaswa kuendelea kuzungumza na nchi hizo zenye nguvu zaidi duniani ili kuumaliza mzozo ulioko wa muda mrefu kuhusu mpango wake wa nyuklia lakini bila ya kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana nchini humo kutokana na mpango huo wa nyuklia.
Khamenei amesema wajumbe wa nchi yake katika mazungumzo hayo wasikubali kushinikizwa kuafikia lolote na kuongeza kuwa Marekani inajua vyema Iran haina nia ya kuunda silaha za kinyuklia.
Iran inataka mazungumzo hayo yafanikiwe ili iondolewa vikwazo ambavyo vimeuathiri vibaya uchumi wake na kurejea kuwa miamba wa kanda.
Mwandishi:Caro Robi/afp/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu