1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo kuhusu Venezuela kuanza tena Norway

29 Mei 2019

Mazungumzo kati ya serikali ya Venezuela na upinzani ya kumaliza mzozo yanatarajiwa kuanza tena Norway huku Washington ikisisitiza suala linalotakiwa kupewa uzito ni kuondolewa kwa rais Nicolas Maduro. 

Venezuela Carabobo Maduro Militärs Marsch der Loyalität
Picha: AFP/HO

Mazungumzo kati ya serikali ya Venezuela na upinzani kuhusu kumaliza mzozo uliodumu kwa miezi kadhaa nchini humo yanatarajiwa kuanza tena nchini Norway, huku Washington ikisisitiza kwamba suala linalotakiwa kujadiliwa kwa uzito kwenye mazungumzo hayo ni kuondolewa kwa rais Nicolas Maduro. 

Wanadiplomasia wa Norway wamesema kwamba pande hizo mbili zitakutana wiki hii nchini Norway, katika mkutano wa kwanza wa ana kwa ana tangu kiongozi wa upinzani nchini Venezuela, Juan Guaido alipojitangaza rais mnamo mwezi Januari. Hata hivyo hawakutaja tarehe wala eneo watakalokutana.

Duru zilizo karibu na mchakato huo, zimeliambia shirika la habari la AFP kwamba mazungumzo hayo yatafanyika mjini Oslo. Hata hivyo, wizara ya mambo ya nje ya Norway haikutaka kuzungumzia suala hilo. Maduro anayeuelezea upinzani kuwa ni "itikadi kali" na wanaofanya kazi kwa niaba ya Marekani, ameahidi kufanya jitihada za kusuluhisha mzozo huo. alisema, "Tutahakikisha tunatumia njia za amani, demokrasia na mshikamano wa kitaifa ili kuondoa utata na mzozo wa Venezuela."

Kiongozi wa upinzani Juan Guaido. Upande wake umekubali kushiriki mazungumzo kwa maelekezo ya Norway.Picha: Imago Images/Agencia EFE

Upande wa upinzani kwa maelekezo ya Norway umekubali kuhudhuria mazungumzo hayo, kufuatia kushindwa kwa mapinduzi ya kijeshi, sambamba na maandamano ya raia ambayo Guaido alitarajia yangesababisha mabadiliko. Guaido anayeungwa mkono na Marekani, anatambuliwa na zaidi ya mataifa 50 kama rais wa mpito.

Katika hatua nyingine, Umoja wa Ulaya nao umeongeza shinikizo la kufanyika kwa uchaguzi mpya wa  rais nchini Venezuela, kama moja ya njia ya kumaliza mzozo unaofukuta nchini humo, baada ya kumteua mwanadiplomasia mahiri na aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya nje wa Uruguay Enrique Iglesias, kuwa mjumbe wake maalumu nchini Venezuela. 

Aliteuliwa kushika wadhifa huo na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja huo, Federica Mogherini. Wanadiplomasia hao wanaamini kwamba Iglesias ambaye ana uraia wa nchi mbili, wa Uruguay na Uhispania, pamoja na uzoefu wa muda mrefu katika mahusiano ya Amerika ya Kusini, atakuw ana nafasi nzuri ya kuzungumza na pande zinazovutana nchini Venezuela.

Aidha, kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitatu, benki kuu ya Venezuela imetoa takwimu za kiuchumi ikisema mfumuko wa bei kwa mwaka 2018, ulifikia asilimia 130,060, wakati uchumi ukiimarika kwa asilimia 47.6 kati ya mwaka 2013 hadi 2018.

Taarifa hizi zinakinzana na zilizotolewa na shirika la kimataifa la fedha, IMF, ambalo lilisema mfumuko wa bei ulipanda hadi asilimia 1,370,000 mwaka jana, kwenye taifa hilo lenye utajiri wa mafuta.