1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo muhimu kuhusu nyuklia ya Iran yaanza

14 Julai 2014

Mazungumzo kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran leo yanaingia katika duru muhimu ya kujaribu kusitisha mpango huo huku wajumbe wa nchi zenye nguvu zaidi duniani pamoja na Ujerumani wakishindwa kuafikiana na Iran.

Picha: REUTERS

Baada ya mawaziri wa nchi za magharibi na Iran hapo jana kushindwa kufikiana mjini Vienna, Austria katika duru ya hivi punde ya kuutafutia ufumbuzi mzozo huo wa mpango wa kinyuklia wa Iran,hii leo waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Marekani John Kerry anatarajiwa kuyaongoza mazungumzo hayo kwa siku ya pili.

Nchi tano zenye nguvu zaidi duniani pamoja na Ujerumani zinatarajia kufikiana makubaliano kamili kuhusu kuusitisha mpango huo tata wa Iran katika kipindi cha siku sita zijazo kwani ndiyo muda wa mwisho uliokuwa umewekwa kuyafikia makubaliano kamili lakini kunaoneka kuibuka tofauti ambazo zinatilia shaka uwezekano huo wa kufikiwa makubaliano katika kipindi hicho cha wiki moja.

Iran yasisitiza ni mpango wa amani

Nchi za magharibi zinataka kufikiwa kwa makubaliano hayo kamili ili kutuliza hofu yao kuwa Iran inapanga kuutumia mpango wake huo kutengeza silaha za kinyuklia,madai ambayo Iran imeyakanusha mara kwa mara na kusisitiza kuwa haikusudii kufanya hivyo bali inataka kuzalisha nishati kwa matumizi ya maendeleo.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry na wa Ujerumanji Frank Walter SteinmeierPicha: REUTERS

Mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza pamoja na wawakilishi kutoka China na Urusi waliwasili jana mjini Vienna wakiwa na matumaini kuwa watakubaliana kuhusu masuala muhimu ambayo yanakwamisha makubaliano kamili kufikiwa.

Hata hivyo hakuna hatua za kuridhisha zilizopigwa hapo jana na mawaziri wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani waliondoka wakisema hakuna mafanikio yaliyopatikana.Hata hivyo Kerry amesalia Vienna kwa ajili ya mazungumzo na mwenzake wa Iran Javad Zarif leo.

Ujerumani yaitaka Iran kufanya maamuzi

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier ambaye alifanya mazungumzo ya moja kwa moja na Zarif alionya kuwa sasa mpira uko upande wa Iran.

Mkuu wa sera za kigeni wa umoja wa Ulaya Bi Catherine Ashton na waziri wa Mambo ya nje wa Iran Javad ZarifPicha: Reuters

Naibu wa waziri wa mambo ya nje wa China Li Baodong amezitaka pande zote kuonyesha nia ya kulegeza kamba huku mjumbe wa Iran Abbas Araqchi akisema katika masuala yote muhimu hakuna upande ulioonyesha kulegeza msimamo.

Kamati ya bunge kuhusu masuala ya kigeni ya Uingereza imesema Rais wa Iran Hassan Rouhani anapaswa kuaminiwa kuhusu mpango huo wa kinyuklia lakini anapaswa kupimwa kutokana na vitendo vyake na sio maneno tu.

Iwapo makubaliano kamili hayatafikiwa ifikapo Jumapili ijayo,pande zote mbili zinaweza kuamua kurefusha muda wa kutekelezwa kwa makubaliano ya muda au kuendelea kufanya mazungumzo.

Mwandishi:Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW