Mazungumzo Syria yaendelea baada ya siku ngumu
24 Januari 2017Mazungumzo hayo yanayoongozwa na Urusi ambayo inaunga mkono utawala wa Syria, na Uturuki inayounga mkono baadhi ya makundi ya upinzani, yalitarajiwa kujikita katika kuuimarisha mpango tete wa usitishaji mapigano nchini kote, ili kuwezesha juhudi pana za kuboresha hali ya kibinadamu nchini Syria.
Mjumbe wa upande wa upinzani Osama Abu Zeid, aliwambia waandishi habari kwamba pande zote zilikuwa zinaendelea kujadiliana ili kuuimarisha mpango wa usitishaji mapigano, na kuongeza kuwa anataraji zaidi ya maneno kutoka kwa Urusi, ambayo ndiyo imekuwa muungaji mkono mkubwa wa utawala wa Syria katika vita hivyo vya umwagaji mkubwa wa damu.
"Nadhani nchi wapatanishi, Urusi na Uturuki zinafanya kazi kuufanya mkutano huu uwe wa mafanikio, lakini kwa hili kutokea kunahitaji kuwepo taratibu za kweli. Kikwazo kikuu kwa ufanisi wa mkutano huu na majadiliano haya ni kuendelea kwa ukiukaji unaofanywa na utawala wa Assad, na kitisho cha watu kulazimishwa kuacha makazi yao katika maeneo mengi ya Syria."
Matumaini ya de Mistura
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria Staffan de Mistura, amesema tangazo la mwisho lilikuwa linakaribia kufikiwa katika mazungumzo hayo yasiyo ya ana kwa ana. "Hatuko mbali na tangazo la mwisho," alisema de Mistura, na kuongeza kuwa mazugumzo hayo hayahusu makaratasi bali usitishaji uhasama, hii ikimaanisha maisha ya Wasyria.
Lakini msemaji wa waasi Yahya al-Aridi amesema mapema leo kuwa kundi hilo lisingesaini tangazo linalotokana na mazungumzo hayo, akisema litatolewa na wadhamini wa mazungumzo, Uturuki inayowaunga mkono waasi, mshirika wa utawala Urusi na yumkini Iran. Aridi aliongeza kuwa tangazo la mwisho lilikuwa ni taarifa ya jumla ambayo haitakiwi kusainiwa na pande zinazoshiriki mazungumzo hayo.
Abu Zeid aliwambia waandishi habari kwamba anadhani mazungumzo hayo yanayofanyika kwenye hoteli ya kifahari ya Rixos katika mji mkuu wa Kazakhstan Astana, huenda yakarefushwa hadi siku ya Jumatano. Mazunguzo hayo yanayohudhuriwa na wajumbe kutoka Urusi, Uturuki, Iran, Marekani na Umoja wa Mataifa, yanalenga kufanikisha utiaji saini makubaliano ya amani.
Malengo yanayokinzana
Waasi walijitoa katika mazungumzo ya ana kwa ana jana Jumatatu wakipinga hatua ya utawala mjini Damascus kuendelea kufanya mashambulizi ya ndege dhidi ya maeneo ya waasi. Upande wa upinzani unasema mazungumzo ya Astana yanapaswa kulenga kuimarisha makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano yalioratibiwa na Urusi na Uturuki mwezi uliopita, lakini utawala unataka suluhisho la kisiasa kwa mgogoro huo, na umewatolea mwito waasi kuweka chini silaha ili wapewe msamaha.
Na habari za hivi punde zinasema Uturuki, Urusi na Iran zimekubaliana juu ya mkakati wa pamoja wa pande tatu kufuatilia ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Syria. Zaidi ya watu 310,000 wameuwa na zaidi ya nusu ya raia wa Syria wamegeuka wakimbizi tangu mgogoro huo ulipozuka mwaka 2011.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,dpae,rtre
Mhariri: Daniel Gakuba