Mazungumzo ya amani kuhusu Sudan Kusini yakwama
8 Januari 2014Pande mbili zinazohasimiana zilikutana kwa mara ya kwanza ana kwana hapo jana mjini Addis Ababa, lakini muda mfupi baadaye, mazungumzo yalisimama ili kutoa fursa kwa wapatanishi wakuu wa Afrika kuelekea Juba kuzungumza na serikali ili kuishawishi kuwaacha wafungwa 11 waliokamatwa mwaka jana kwa tuhuma za kujaribu kuipindua serikali.
Hata hivyo, serikali ya Rais Salva Kiir imekatalia mbali ombi hilo la waasi na kusema wafungwa hao wataachiliwa tu baada ya taratibu kamili za kisheria kufuatwa.
Wapatanishi hao waliokwenda kumzungumzia Kiir ni wa kutoka jumuiya ya ushirikiano wa nchi za Afrika Mashariki na pembe ya Afrika IGAD ambao ndiyo wanaoongoza mazungumzo hayo na wanatarajiwa kurejea mjini Addis Ababa leo jioni.
Hatma ya mazungumzo ni ati ati
Haijulikani iwapo wajumbe wanaowakilisha upande wa waasi watajiondoa kutoka meza ya mazungumzo baada ya serikali kukataa matakwa ya kuwaachia wafungwa wa kisiasa au la.
Kiongozi wa wajumbe wa serikali Michael Makuei amesema IGAD imewasilisha mapendekezo ya kusitishwa kwa vita ili kumaliza mzozo ulioko na pande zote mbili zitajadili misimamo yao leo.
Mapigano yaliyoanza tangu tarehe 15 mwezi Desemba ndiyo mabaya zaidi kuwahi kulikumba taifa hilo changa zaidi duniani tangu lilipojinyakulia uhuru mwaka 2011. Na huku mamia ya watu wakiandamana leo mjini Juba: kuna matumaini finyu kuwa mzozo huo utapata ufumbuzi hivi karibuni.
Mzozo huo umezuka kufuatia tofauti za kisiasa kati ya Rais Kiir na aliyekuwa makamu wake Riek Machar na kugeuka mapigano ya kikabila kati ya Dinka na Nuer.
Msemaji wa upande wa Machar Brigedia Jenerali Lul Raui Kong amesema kwa hivi sasa kuna makabiliano makali ya kijeshi kati ya wapiganaji wa waasi wa wanajeshi wa serikali kuudhibiti mji wa Bor.
Uganda yajiingiza katika mzozo wa Juba?
Kong ameongeza kuwa Uganda imetuma wanajeshi 1,200 kulinda maeneo muhimu nchini Sudan Kusini kama uwanja wa ndege na Ikulu ya Rais. Uganda imesema kutumwa kwa wanajeshi wake mjini Juba ni kufuatia ombi la Rais Kiir.
Msemaji wa jeshi la Uganda Kanali Paddy Nkunda amesema leo kuwa wanajeshi hao waliotumwa jana na juzi, walipelekwa ili kukidhia mapungufu ya ya kiusalama ya Sudan Kusini na kukanusha kuwa nchi yake inahusika katika mapigano yanayoendelea.
Rais wa Uganda Yoweri Museveni ni mshirika wa karibu wa Kiirna hivi karibuni Museveni alimuonya Machar kuwa nchi za Afrika Mashariki zitaungana kumshinda iwapo hatakubali kushiriki katika mazungumzo ya amani.
Mwandishi: Caro Robi/Reuters/ap
Mhariri: Mohammed Khelef