1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani Ukraine yarejea

7 Machi 2022

Wapatanishi katika mzozo kati ya Urusi na Ukraine wameanza awamu ya tatu ya mazungumzo nchini Belarus hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la Urusi, RIA, baada ya awamu mbili za mwanzo kushindwa.

Demo Stoppt den Krieg! in Berlin
Picha: Marc Vorwerk/SULUPRESS.DE/picture alliance

Awamu hii ya tatu ya mazungumzo inafuatia mbili za mwanzo zilizoshindwa kuutatua mzozo huo huku kila upande ukimtupia lawama mwenzake kwa kushindwa kupata makubaliano yanayofaa katika mzozo huo ulioingia siku ya 12 hii leo. 

Soma Zaidi: Ukraine yasema Urusi inakiuka makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda

Mazungumzo yaliyofanyika Alhamisi iliyopita yalimalizika kwa pande hizo mbili kukubaliana kufungua njia salama za raia kuondoka kwenye miji iliyozingirwa, ingawa majaribio mawili ya kusitisha mapigano ili kufungua njia hizo Jumamosi na Jumapili yalidumu kwa masaa kadhaa tu na kusababisha raia kwa maelfu kubakia kwenye miji hiyo bila ya maji, chakula wala umeme.

Mjumbe wa mazungumzo hayo kutoka Ukraine Mykhailo Podolyak kabla ya kuanza mazungumzo hayo ameitolea mwito Urusi kusimamisha mashambulizi dhidi ya raia.

Mapema leo, Urusi ilitangaza kuwafungulia njia raia wa Ukraine waliopo katika majiji yaliyozingirwa kupita kwenda Urusi, hatua iliyokosolewa vikali yaUkraine ikisema ni ya kujionyesha tu huku rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akisema ni unafiki mtupu. Macron amekiambia kituo cha televisheni cha LCl kwamba hajui ni WaUkraine wangapi wanataka kukimbilia Urusi.

Kumekuwepo na taarifa za kukinzana, wakati Ukraine ikidai kwamba raia wanazuiwa kupita kwenye njia hizo kutokana na mashambulizi ya Urusi, huku baadhi ya maafisa nchini humo wakidai, raia hao wanaondoka bila ya shida yoyote.

Soma Zaidi: Juhudi za kuwahamisha wakaazi wa Mariupol zashindwa tena

Umoja wa Ulaya umeiomba china kuingilia kati kwa kumshawishi rais Vladimir Putin kusimamisha mashambulizi nchini Ukraine.

Wakati wasiwasi ukizidi kuongezeka, tume ya Umoja wa Ulaya umeitolea mwito China kuchukua jukumu la usuluhishi, kwa kuishawishi Urusi kuvimaliza vita hivyo. Msemaji wa tume hiyo Peter Stano amesema China ina uwezo mkubwa wa kufanya hivyo kutokana na mahusiano baina ya mataifa hayo.

Amesema, "China ina uwezo mkubwa wa kuifikia Urusi kutokana na mahusiano yao na tungependa China kutumia ushawishi wake kuishinikiza Urusi kusitisha mapigano na kumaliza hatua za kikatili, mashambulizi yaliyopitiliza na mauaji ya raia nchini Ukraine."

Nchini Uturuki, waziri wa mambo ya nje Mevlut Cavusoglu ametangaza huenda wakakutana na wenzake wa Urusi Sergey Lavrov na wa Ukraine Dymitro Kuleba baadae wiki hii. Mikutano baina yao inaweza kufanyika pembezoni mwa kongamano la kidiplomasia la Antalya na mazungumzo yao yakitarajiwa kuwa ya ngazi za juu zaidi kufanyika tangu Urusi ilipoivamia Ukraine.Uturuki ina mahusiano thabiti mataifa hayo yote mawili.

Na huko London tunaarifiwa kwamba bei ya jumla ya gesi barani Ulaya na Uingereza imefikia kiwango cha juu kabisa hii leo, wakati kukiwa na wasiwasi wa Urusi kuwekewa vikwazo vya kuuza nishati nje, kufuatia uvamizi huo. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Anthony Blinken pamoja na washirika wa Ulaya walikuwa wanaangazia kuizuia Urusi kuyauzia mafuta mataifa hayo, hatua iliyochochea ongezeko hilo  ambalo halijashuhudiwa tangu mwaka 2008.

Na huko Washington, taarifa zinasema rais Joe Biden amepanga kufanya mazungumzo na viongozi wa Ufaransa, Uingereza na Ujerumani hii leo kujadiliana mambo yalivyo nchini Ukraine.

APE/DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW