Mazungumzo ya Amani ya Mashariki ya Kati Yakwama
25 Aprili 2014"Daima kunaibuka uwezekano wa kusonga mbele." anasema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani.Hata hivyo John Kerry anahisi waisrael na wapalastina wanabidi wafikie maridhiano ili mazungumzo yaliyoanza miezi tisa iliyopita yaweze kuendelea baada ya April 29 ijayo-wakishindwa anasema na hapa tunanukuu" basi amani haitakua rahisi kupatikana".
"Kamwe hatutakata tamaa au kuachilia mbali jukumu letu la kusaka amani" ameshadidia waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani.
Maamuzi kadhaa yamepitishwa katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita na pande zote mbili ,Israel na Palastinaa na kuzidi kukorofisha mazungumzo ya amani ambayo tokea hapo ni tete .
Serikali ya Suluhu ya Wapalastina ndio Mzizi wa Fitina
Msemaji wa wizara hiyo Jen Psaki amesema John Kerry amezungumza na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas na kumuelezea msimamo wake dhidi ya mipango ya kuundwa serikali ya suluhu pamoja na Hamas-wanaotajwa na Marekani ,Umoja wa Ulaya na wengineo kuwa ni magaidi.
Hapo awali waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema"kamwe hatojadiliana na serikali ya Palastina inayowajumuisha watu wanaotoa wito wa kuteketezwa Israel."Benjamin Netanyahu anamtuhumu Mahmoud Abbas kuwatanguliza mbele Hamas badala ya amani."
Hata hivyo mkuu wa tume ya Israel katika mazungumzo ya amani bibi Tzipi Livni ambae ni waziri wa sheria wa Israel ameelezea matumaini yake kuona ufumbuzi unapatikana ili mazungumzo yaendelee.
Duru mpya ya mazungumzo ya amani iliyoanza msimu wa kiangazi mwaka jana,ilikuwa imalizike April 29 ijayo kwa kupatikana makubaliano ya kuundwa madola mawili.
Marekani haijakata Tamaa
Tangu wakati huo hakuna makubwa yaliyofikiwa na wanadiplomasia walikuwa wakijitahidi kutafuta ridhaa ili mazungumzo yaendelee kwa miezi kadhaa mengine baada ya April 29.
Haijulikani bado kwa muda gani Marekani inapanga kuachilia kizungumkuti hiki kiendelee.Kilichodhahir na kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani, Jen Psaki , wapatanishi wa Marekani watasalia angalao kwa sasa katika eneo hilo.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman