1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani ya Syria yako hatarini

Oumilkheir Hamidou
4 Januari 2017

Uturuki inasema visa vinavyoyaendeya kinyume makubaliano ya kuweka chini silaha nchini Syria vinatishia kukorofisha mazungumzo ya amani nchini Kazakhstan.

Syrien Assad Regime verletzt Waffenruhe in Aleppo
Picha: picture alliance/dpa/AA/A. al Ahmed

Akizungumza na shirika la habari linalomilikiwa na serikali Anadolu, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu ameitolea wito Iran iwashinikize wanamgambo wa shia na vikosi vya serikali ya Syria waache kuyaendeya kinyume makubaliano ya kuweka chini silaha. Ameonya visa kama hivyo vinatishia kuyatia hatarini mazungumzo ya amani.

Uturuki inashirikiana na Urusi katika masuala ya kuwekewa vikwazo wale wote wanaovunja makubaliano ya kuweka chini silaha. Makubaliano hayo yamelengwa kufungua njia ya kuitishwa mazungumzo ya amani baadae mwezi huu mjini Astana nchini Kazakhstan kati ya wawakilishi wa serikali ya mjini Damascus na wale wa upande wa upinzani.

Wakaazi wa Damascus wanasumbuliwa na ukosefu wa majiPicha: picture-alliance/dpa/Y. Badawi

Maafisa wa serikali ya Urusi wanatarajiwa kufika ziarani nchini Uturuki kuanzia Januari tisa hadi kumi, kuzungumzia ratiba ya mazungumzo hayo ya amani.

Onyo la waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki Cavusoglu limetolewa baada ya makundi kadhaa ya waasi kusema wanajitoa katika maandalizi ya mazungumzo ya amani, wakiilaumu serikali ya Syria kuvunja makubaliano ya kuweka chini silaha kwa kulihujumu eneo la Wadi Barada umbali wa kilomita 15 karibu na mji mkuu Damascus.

Waasi wanaikosoa serikali kwa kuyaendeya kinyume kila mara makubaliano ya kuweka chini silaha.

Shirika linalosimamia masuala ya haki za binaadam limethibitisha na kusema vikosi vinavyoiunga mkono serikali vikisaidiwa na wanamgambo wa Hisbollah wameendelea kulishambulia eneo la Wadi Barada, eneo muhimu inakokutikana shehena kubwa ya maji ya kunywa kwa ajili ya wakaazi milioni nne wa mji mkuu Damascus na vitongoji vyake.

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu (kushoto) na Urusi Sergei Lavrov (kulia)Picha: picture-alliance/dpa/M. Shipenkov

 Shirika linalosimamia masuala ya haki za binaadam laonya makubaliano ya kuweka chini silaha yako hatarini

Serikali ya Rais Bashar al Assad inawatuhumu waasi kunyunyizia mafuta ya dizel ndani ya visima hivyo vya maji na kuyafunga mabomba yanayosafirisha maji safi hadi mji mkuu ambao tangu Disemba 22 unakabiliwa na ukosefu wa maji. Waasi wanahoji hujuma za serikali ndio chanzo cha kupasuka mabomba ya maji.

Mwenyekiti wa shirika hilo linalosimamia masuala ya haki za binaadam lenye makao yake nchini Uingereza, Rami Abdel Rahman anaonya pia makubaliano ya kuweka chini silaha "yako hatarini" na yanatishia kuvunjika ikiwa Urusi na Uturuki hazitoingilia kati kuyanusuru.

 

Mwandishi: Hamidou Oumilkheir/ Reuters/ AFP/AP

Mhariri: Grace Patricia Kabogo