1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani ya Urusi na Ukraine yameanza Uturuki

29 Machi 2022

Wajumbe wa timu za kutafuta suluhu ya vita vya Ukraine na Urusi leo hii wamerejea tena katika mkutano wao ana kwa ana mjini Istanbul, Uturuki

Türkei | Verhandlungen zwischen Russland und der Ukraine in Istanbul
Picha: Turkish Presidency via AP/picture alliance

Mazungumzo hayo yanaendelea huku Ukraine ikianzisha upya jitihada za uokozi wa watu katika miji yake inayodhibitiwa na Urusi pamoja na kupambana vikali katika kuudhibiti mji wa bandari uliozingirwa wa Mariupol.

Mazungumzo ya sasa yanafanyika kwa uhudhuriaji wa siku ya mwanzo wa Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, na kukiwa na manug'uniko kuwa mkutano wa mwanzo ulivurugwa kwa manaeno yasio ya kweli. Kabla ya mkutano huo unaofanyika katika makazi yake, Erdogan alitoa wito wa kuyafikisha mwisho mapigano, akisema Urusi na Ukraine zote zina mashaka halali kabisa kwa maslahi ya kila nchi.

Katika ufunguzi wa mazungimzo hayo Erdogan alisema "Uturuki haikwepi kuwajibika kwa ajili ya amani na utulivu wa kikanda na kimataifa, na kamwe haitofanya hivyo. Tunaamini hakuna atakaepoteza chochote kwa kuzungumzia  juu ya uhalali wa amani. Na kurefusha vita hakuna faida kwa yeyote. Ni ndani ya dhamira za pande hizi mbili upo uwezekano kufikisha ukomo wa janga hili." Alisema rais huyo.

Erdogan asisitiza umuhimu wa kusitishwa mapigano

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na wajumbe wa Urusi na UkrainePicha: DHA

Mbele ya wajumbe wa mkutano huo, rais Erdogan ameongeza kusema ni muhimu kwa pande hizo kukubaliana juu ya usitishwaji wa vita. Na kuongoza kuwa anaamini kwa pamoja wapo katika mchakato wa kufanikisha azimio thabiti na madhububuti huku akiwakumbusha kuwa ulimwengu mzima unategema habari njema kutoka kwao.

Katika hatua nyingine Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi, Igor Konashenkov amesema Urusi itaendeleza uhasama wake dhidi ya Ukraine pamoja na kuendelea kwa mkutano wa Istanbul.

Katika taarifa ambayo haijathibitishwa, imeelezwa kwamba mashambulizi ya anga ya Urusi yameteketeza vifaa 68 vya kivita vya Ukraine. Miongoni mwa vifaa hivyo ni pamoja na mifumo ya kujikinga na makombora, vituo vya mafuta na ndege tatu zinazorushwa bila ya rubani.

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA), Rafael Grossi awasili nchini Ukraine

Ndani nchini Ukraine, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA), Rafael Grossi yupo nchini humo kwa lengo la kufanya mazungumzo na maafisa wa serikali kwa shabaha ya kuhakikisha usalama na ulinzi wa maeneo ya nishati ya nyuklia. Kiongozi huyo pia wiki hii anatarajiwa kutembelea moja kati ya vinu vya nyuklia vya taifa hilo.

Wakati Shirika la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR likisema limefanikiwa kuwaokoa watu laki tisa nchini humo, Shirikla la Afya WHO nalo linaripoti kuuwawa kwa watu 72 na 40 kujeruhiwa katika mashambulizi ambayo yamefanywa katika maeneo ya vituo vya afya.

Ni zaidi ya mwezi sasa tangu vifaru vya  Rais wa Urusi kuingia katika ardhi ya Ukraine, wakiwa na matumaini ya kuidoofisha au kuiondoa kabisa madarakani serikali halali ya mjini Kyiv. Hadi wakati huu mapigano yanakadiliwa kusababisha wakimbizi zaidi ya milioni 10, na kwa mujibu wa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky pia yamesababisha vifo vya takribani watu elfu 20.

Vyanzo: RTR/AFP/DPA

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW