Mazungumzo ya amani yakwama, M23 na serikali zikijiimarisha
7 Oktoba 2025
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na waasi wa AFC-M23 zimeonekana kujizatiti kijeshi katika kile kinachoelezewa na wachambuzi kama mbinu ya kujiongezea ushawishi kwenye meza ya mazungumzo.
Mbinu hiyo inajumuisha kauli kali kutoka kila upande ambapo waasi wanatishia kuiangusha serikali ya Rais Felix Tshisekedi vitisho ambavyo wasaidizi wa kiongozi huyo wamevilinganisha na ndoto ya mchana.
Wiki mbili tu baada ya waasi wanaodhibiti sehemu kubwa ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kusajili zaidi ya wapiganaji wapya 7,000, karibu wapiganaji wengine 9,000 wamehitimisha mafunzo yao wiki iliyopita.
Katika sherehe ya kuhitimisha mafunzo ya kijeshi ya wapiganaji hao wapya jana huko Tchanzu, katika jimbo la Kivu Kaskazini, kamanda mkuu wa waasi wa M23 Jenerali Sultani Makenga, alitangaza azma ya waasi hao kuangusha kile alichokiita "utawala mbovu” wa Kinshasa.
UDPS: Tshisekedi hawezi kupinduliwa na 'vikaragosi'
Lakini kwa chama cha UDPS cha Rais Félix Tshisekedi, tishio hilo halina maana yoyote. Christian Lumu Lukusa ni mmoja wa viongozi wa chama hicho aliyesema,
"Rais Tshisekedi hawezi kupinduliwa na vikaragosi vinavyopokea amri kutoka Kigali au kwingineko. Kuhusu madai yao ya kuongeza idadi ya wapiganaji, wajue kuwa DRC si uwanja wa michezo. Serikali iko tayari jeshi la FARDC liko tayari na pia wananchi wako tayari. Wananchi wameazimia kumaliza upuuzi huu wote. Tutausambaratisha uasi huu muda si mrefu."
Kauli hizi zinatolewa wakati mazungumzo kati ya serikali ya Kongo na waasi wa AFC-M23 yakitarajiwa kuanza tena wiki hii huko Doha, Qatar. Yvon Muya, mtafiti katika chuo cha masuala ya mizozo cha Saint-Paul huko Ottawa, Canada, anasema kauli hizi zinalenga kuimarisha nguvu ya kila upande katika meza ya mazungumzo.
"Kila upande unaendelea kujipanga kimkakati, kimsingi kujiimarisha kivita inamaanisha kuimarisha hoja na misimamo kwenye meza ya mazungumzo. Tunaona hilo kupitia kauli zinazotolewa. Pia mbinu hii ya kutoleana maneno ya vitisho ni ya kawaida katika mchakato wa amani unaofanyika katika muktadha wa kijeshi. Hali ambayo tunaiona sasa, kwani mapigano yanaendelea."
'Mazungumzo ya Doha hayajapiga hatua' mtaalamu
Kulingana na Henri-Pacifique Mayala, mtafiti katika Taasisi ya Ebuteli huko Kivu mazungumzo ya mjini Doha bado hayajaweza kupiga hatua huku mizani ya nguvu ikionekana kutobadilika kwenye mstari wa mbele wa vita.
"Uwezekano mkubwa ni kuendelea kwa hali ilivyo sasa ikiwa mazungumzo yatashindwa kupiga hatua. Suluhisho la kijeshi halijawahi kuondolewa katika mikakati ya kila upande katika mzozo huu. Lakini ningetarajia zaidi kuendelea kwa hali ya sasa ilivyo badala ya kutazamia mabadiliko katika uwanja wa mapambano; kama vile jeshi kuwafurusha waasi au waasi kuyapanua zaidi maeneo wanayoyadhibiti."
Waasi hao wanaoungwa mkono na Rwanda wanashikilia miji ya Goma na Bukavu ambayo ni makao makuu ya mikoa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini na pia vijiji na miji kadhaa midogo katika mikoa hiyo ya mashariki mwa Kongo.