1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpatanishi mkuu wa serikali arejea nyumbani baada ya tukio

11 Januari 2018

Rais wa Colombia Juan Manuel Santos amesema mashambulizi mapya yaliyofanywa na waasi hapo jana yamesababisha kumuita mpatanishi wake mkuu katika mazungumzo ya amani na waasi wa mwisho waliobakia nchini humo.

Großbritannien Präsident Juan Manuel Santos in London
Picha: picture-alliance/abaca/K. Green

Ripoti ya machafuko yaliyofanyika hapo jana imetolewa saa kadhaa baada ya kumalizika kipindi cha kusimamisha mapigano, kilichokubaliwa na Umoja wa Mataifa, viongozi wa kidini na maafisa wa serikali, kilichosifiwa kama hatua muhimu ya kupunguza vurugu na kuelekea mwisho wa mgogoro kati ya serikali na waasi.

Waasi wa National Liberation Army, ELN, na wajumbe wa serikali kwa pamoja walielezea matumaini ya kufikia makubaliano mapya ya kurefusha kipindi cha kusimamisha mapigano katika mazungumzo mapya yaliyotarajiwa kuanza siku ya Jumatano nchini Ecuador.

Akizungumza katika hotuba fupi kupitia televisheni ya taifa nchini Colombia, Rais Juan Manuel Santos alisema kundi hilo la waasi sio tu lilikataa kuingia katika duru mpya ya mazungumzo, lakini walitekeleza shambulio la kigaidi, lililosababisha vifo vya watu 14 siku ambayo mazungumzo mapya yalitarajiwa kuanza.

Rais Juan Manuel Santos akimsikiliza mmoja wa wanachama wa kundi la waasi la ENLPicha: picture-alliance/dpa/C.Escobar Mora

Rais Santos amesema hilo lilimfanya amuombe mpatanishi wake mkuu, Gustavo Bell kuondoka mara moja na kurejea nyumbani ili kutathmini mipango ya baadaye ya mazungumzo hayo.

Pia rais huyo wa Colombia aliliagiza jeshi la Colombia kujibu vikali uchokozi uliotekelezwa na waasi. Aidha hatua imerejesha nyuma juhudi za kumaliza vurugu za kisiasa zilizodumu nusu karne katika taifa hilo la Amerika ya Kusini. 

Muda mfupi baada ya tangazo hilo wizara ya ulinzi ilitangaza kuwazuwia wanachama wawili wa kundi la waasi la ELN na kuwashtaki kwa makosa ya kumiliki silaha na kufanya shambulio la kigaidi. Kwa upande wao wajumbe wa waasi wa ELN wamesema shambulizi limetokea wakati wa mgogoro na haipaswi kusimamisha shughuli za upatanishi. Msemaji wa kundi hilo amesema kuitwa kwa mpatanishi mkuu wa serikali hakumaanishi mazungumzo yamevunjika bali wanachukulia kama njia moja ya mashauriano

Katika juhudi za kufanikisha mazungumzo ya amani yanayoonekana kuyumba, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres atasafiri kuelekea Colombia mwishoni mwa juma hili wakati kukiwa na wasiwasi kuhusu kujumuishwa kwa kundi kubwa la waasi na mashambulizi mapya yanayofanywa na kundi la mwisho la waasi la ELN.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/dpa/AP/ Reuters

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW