1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Brexit yaanza Brussels

19 Juni 2017

Katika siku ya kwanza ya duru ya kwanza ya mazungumzo hayo, pande zote mbili zimetilia mkazo haja ya kukabiliana na hali ambazo bado hamna uhakika ili kujenga nia ya kuafikia mkataba ulio mzuri kwa wote.

Picha: Reuters/F. Lenoir

Wajumbe wanaojadili mchakato wa Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya wakiongozwa na washauri wawili wakuu kutoka pande zote mbili, leo wameanza duru ya kwanza ya mazungumzo mjini Brussels Ubelgiji kuhusu hatua za Uingereza kujiondoa kwenye umoja huo.

Katika siku ya kwanza ya duru ya kwanza ya mazungumzo hayo, pande zote mbili zimetilia mkazo haja ya kukabiliana na hali ambazo bado hamna uhakika ili kujenga nia ya kuafikia mkataba ulio mzuri kwa wote. Waziri wa Uingereza wa masuala ya utengano huo - Brexit David Davis ameongeza kuwa wameanza mazungumzo kwa nia njema wakiwa tayari kujenga ushirikiano imara na maalum kati yao na washirika kutoka Ulaya na marafiki katika siku za baadaye. Davis anaendelea kusema "Yapo masuala mengi yanayounganisha Umoja wa Ulaya na Uingereza kuliko yale yanayotutenganisha. Kwa hivyo japo kutakuwa na changamoto mbele yetu katika mazungumzo, tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha tunapata maelewano kwa manufaa ya masilahi ya raia wetu.

Mwakilishi Mkuu wa mazungumzo hayo kwa upande wa Umoja wa Ulaya Michel Barnier, amesema anayo matumaini kuwa katika mazungumzo hayo yanayoanza takriban mwaka mmoja tangu Uingereza kupiga kura ya kujitenga na Umoja wa Ulaya, wataweza kuafikiana kuhusu ratiba ya jinsi mazungumzo yatafanywa. Barnier anaongeza kuwa "Lengo letu liko wazi. Ni lazima tukabiliane na ukosefu wa uhakika ambao umesababishwa na Brexit.-Kwanza kwa raia na pia kwa watakaonufaika kutokana na sera za Umoja wa Ulaya na kwa athari kuhusu mipaka hususan Ireland. Ninatumai leo tutaweza kutambua vipaumbele na ratiba."

Wajumbe wa EU na Uingereza wanaoshiriki mazungumzo ya BREXITPicha: picture-alliance/AP Photo/E. Dunand

Misukosuko dhidi ya Theresa May

Wapatanishi kutoka pande zote mbili walikubali kuendelea na mazungumzo jinsi yalivyopangwa awali. Haya yanajiri wakati ambapo Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May akikabiliana na misukosuko ya kisiasa baada ya chama chake cha Conservative kushindwa kupata wingi wa viti bungeni kwenye uchaguzi ulioitishwa mapema.

Uingereza ambayo imekuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya tangu mwaka 1973 ndiyo nchi ya kwanza kujitenga na Umoja huo kufuatia kura ya maoni. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema Umoja wa Ulaya itasikiliza kwa umakini matakwa ya Uingereza kwa manufaa ya pande zote mbili ili kuafikia mkataba mzuri. Naye Waziri wa nchi za nje wa Uingereza Boris Johnson ambaye alifanya kampeni ya utengano huo, amesema anatarajia maelewano yenye furaha kutokana na mazungumzo hayo yanayofanyika Brussels Ubelgiji.

Mwandishi: John Juma/DPAE/RTRE

Mhariri: Josephat Charo