Mazungumzo ya Hamas na wapatanishi yaanza vyema
7 Oktoba 2025
Juhudi hiyo inafanyika wakati Rais wa Marekani Donald Trump akisema kuwa kundi la wapiganaji wa Kipalestina liko tayari kufanya maridhiano kuhusu mapendekezo yake ya makubaliano ya amani.
Al-Qahera News, chombo kinachohusishwa na ujasusi wa serikali ya Misri, kilisema duru ya kwanza ya mazungumzo ilimalizika "katika mazingira chanya" na inaendelea tena Jumanne hii.
Kwa faragha na chini ya ulinzi mkali, wajumbe walitarajiwa kuzungumza kupitia wapatanishi kati ya pande hizo, ikiwa ni wiki chache tu baada ya Israel kujaribu kuwaua wajumbe wakuu wa Hamas katika shambulio huko Qatar. Al-Qahera News awali ilisema wajumbe walikuwa "wakijadili maandalizi ya mazingira ya kuachiliwa kwa waliokamatwa na wafungwa".
Taarifa ilisema "Upatanishi wa Misri na Qatarunafanya kazi na pande zote mbili kuanzisha utaratibu" wa kuwaachilia mateka walioko Gaza kwa kubadilishana na Wapalestina walioko magerezani Israel.
Trump aliwaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya White House kuwa alikuwa "na uhakika kiasi" kuwa makubaliano ya amani yanawezekana.
Merz aonya kuhusu kuongezeka kwa chuki dhidi ya Wayahudi
Katika kumbukumbu ya miaka miwili tangu mauaji ya Oktoba 7 yaliyofanywa na kundi la Hamas nchini Israel, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito kwa Hamas na Israel kusitisha vita vya Gazamara moja. Akisema pendekezo jipya la Rais Trump linatoa fursa ya kumaliza mgogoro huo. Aidha katika kipindi cha kumbukumbu hiyo pia Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz ametahadharisha juu ya kuongezeka kwa visa vya chuki dhidi ya Wayahudi nchini Ujerumani.
Vatican yalaani mauaji ya kutisha yanayoendelea Gaza
Mwanadiplomasia Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Kardinali Pietro Parolin, amelaani vikali "mauaji" yanayoendelea Gaza na kusema ni jambo "lisilokubalika" kupuuza idadi ya vifo huko kwa kuzona kama athari zitokanazo kandoni mwa vita.
Parolin alisema vita kati ya Hamas na Israel "vimesababisha madhara makubwa na ya kikatili", akiongeza kuwa ameguswa sana na idadi ya vifo vya kila siku miongoni mwa Wapalestina, wakiwemo "watoto wengi ambao kosa lao pekee ni kuzaliwa mahali hapo".