1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Iran na mataifa 6 yenye nguvu, yapiga hatua

31 Desemba 2013

Mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran kati ya nchi hiyo na mataifa sita yenye nguvu duniani yamepiga hatua kuhusu namna ya kuutekeleza mkataba wa kupunguza urutubishaji wa madini ya uranium.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas AraqchiPicha: ISNA

Mkataba huo pia utaiwezesha Iran kupunguziwa vikwazo vya kiuchumi. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi amesema leo kuwa mazungumzo hayo ya wataalamu wa Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani yamepiga hatua ingawa bado masuala kadhaa yanahitaji kutatuliwa katika ngazi ya kisiasa. Hata hivyo, Araqchi ambaye ni mpatanishi msaidizi wa Iran, hajafahamisha wazi jinsi pande hizo mbili zilivyotatua masuala kadhaa ya kiufundi yaliyoainishwa katika mkataba uliofikiwa kwenye mazungumzo ya Geneva Novemba 24 mwaka huu wa 2013.

Wataalamu kutoka Iran na mataifa matano yenye uwanachama wa kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambayo ni Urusi, China, Ufaransa, Uingereza na Marekani pamoja na Ujerumani, walianza mkutano wao jana Jumatatu mjini Geneva na kumalizika leo asubuhi (31.12.2013). Kwa pamoja mataifa hayo saba yanataka kuanza kuutekeleza mkataba wa Novemba ifikapo mwishoni mwa mwezi Januari, kwa kipindi cha miezi sita na hivyo kuweka muda kwa ajili ya makubaliano ya kina zaidi.

Mkutano huu ni wa tatu kufanyika tangu kufikiwa kwa mkataba huo wa Novemba 24 mwaka huu, kwa lengo la kuufanyia kazi utekelezaji wake. Akizungumza na shirika la habari la taifa la Iran-IRNA, Araqchi amesema kuwa wataalamu hao watawasilisha ripoti zao kwa wakurugenzi wa kisiasa kwa sababu baadhi ya masuala yaliyobakia yanahitaji kutatuliwa katika ngazi za kisiasa.

Baadhi ya viongozi wa mataifa sita yenye nguvu duniani pamoja na IranPicha: Reuters

Umoja wa Ulaya waratibu mawasiliano

Maafisa wa Umoja wa Ulaya ambao wanaratibu mawasiliano na Iran kwa niaba ya mataifa hayo sita yenye nguvu duniani, wamekataa kuzungumzia matokeo ya mkutano huo hadi sasa. Araqchi amesema anatarajia kukutana na naibu mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Helga Schmid, kujadiliana masuala kadhaa wiki ijayo.

Mazungumzo hayo ya kiufundi yalianza Desemba 9, lakini Iran iliyakwamisha kwa muda baada ya Marekani kuyaorodhesha makampuni 19 ya Iran na watu binafsi katika orodha ya makumpuni yaliyowekewa vikwazo kwa sasa. Maafisa wa Iran walisema kuwa hatua hiyo ilikiuka juhudi za kuutekeleza mkataba huo, lakini maafisa wa Marekani wamesema kuwa haijakiuka makubaliano.

Mataifa hayo sita yenye nguvu duniani yakiongozwa na Marekani yanahofu kuwa mpango wa nyuklia wa Iran ni kwa ajili ya kutengeneza silaha za atomiki na hivyo kuiwekea nchi hiyo vikwazo katika juhudi za kuilazimisha Iran iachane na mpango wake huo wa nyuklia. Hata hivyo, Iran imekuwa ikikanusha madai hayo na kusema kuwa mpango wake huo ni kwa ajili ya matumizi salama hasa katika matumizi ya nishati ya umeme na utafiti wa kimatibabu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE,RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW