1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya kufufua mkataba wa nyuklia wa Iran kuanza tena

29 Novemba 2021

Mazungumzo juu ya kufufua mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 uliofikiwaikiwa kati ya Iran na mataifa makubwa, yanatarajiwa kuanza tena Jumatatu mjini Vienna Austria. Lakini matumaini ya kupatikana maelewano ni madogo.

Österreich | Internationale Atomenergie-Organisation | Iran Atomstreit
Picha: Thomas Kronsteiner/Getty Images

Miezi mitano tangu duru ya mwisho ya mazungumzo hayo, wanadiplomasia wa ngazi ya juu kutoka Ujerumani, Ufaransa, Urusi, Uingereza na China, wanarudi tena mjini Vienna kwa awamu nyingine ya majadiliano kati yao na wawakilishi wa Iran na Marekani.

Lakini hayo yanapojiri kuna hali ya kutoaminiana. Mkuu wa mashauriano anayewakilisha Iran Ali Bagheri amesema hawafikiri mataifa ya Magharibi yako tayari kwa makubaliano.

Naye mkuu wa mashauriano upande wa Marekani Robert Malley hivi karibuni alisema watachukua msimamo mkali iwapo Iran haitalegeza kamba. Kauli hizo zinamaanisha kwamba huenda suluhisho la haraka lisipatikane.

Lengo la mazungumzo hayo ni lipi?

Mkuu wa mashauriano wa Iran Ali Bagheri (kulia) na mratibu wa masuala ya nyuklia wa Umoja wa Ulaya Enrique Mora.Picha: Iranian Foreign Ministry/ZUMA/picture alliance

Lengo la mazungumzo hayo ni kunusuru makubaliano ya kimataifa ya mwaka 2015, yanayojulikana pia kama (JCPOA), ambayo yaliweka masharti kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, ili kuizuia nchi hiyo isiweze kutengeneza silaha za kinyuklia.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, vizuizi ambavyo nchi za Magharibi ziliiwekea Iran viliondolewa.

Lakini mnamo mwaka 2018, Marekani chini ya rais wake wa Zamani Donald Trump iliondoka kwenye makubaliano hayo, na badala yake ikarudisha vikwazo dhidi ya Iran hivyo kuathiri uchumi wa taifa hilo.

Kutokana na hilo, Iran iliamua kutanua shughuli zake za kinyuklia na kurutubisha zaidi madiniya urani kiasi cha kufikia kiwango kinachoweza kutengeneza silaha. Isitoshe iran ilipunguza ruhusa kwa ukaguzi wa kimataifa wa shughuli zake hizo.

Japo mashauriano hayo yanaanza leo, wachambuzi wanasema vipo vizingiti vingi tangu awamu ya mwisho ya majadiliano mwezi Juni.

Rafael Grossi: Masuala tete yangalipo

Mtizamo umebadilika pakubwa tangu kuingia madarakani kwa rais mhafidhina nchini Iran Ebrahim Raisi.

Mkuu wa shirika la IAEA Rafael GrossiPicha: Lisa Leutner/AP Photo/picture alliance

Kwa miezi kadhaa sasa, Iran imepuuza miito ya mataifa ya magharibi kutaka mazungumzo hayo kuanzishwa huku ikiendelea kuimarisha uwezo wake kupitia mpango wa nyuklia.

Wiki iliyopita, mkuu wa shirika linalosimamia matumizi ya nguvu za atomiki (IAEA) Rafael Grossi, aliizuru Iran kujaribu kupiga msasa baadhi ya masuala tete kati ya shirika lake na nchi hiyo.

Lakini baada ya ziara hiyo, alisema hakuna mafanikio yaliyopatikana kuhusu masuala aliyoibua.

Marekani imesema ikiwa mkwamo utadumu basi itaitisha mkutano maalum wa bodi ya (JCPOA) mwezi Disemba

Kelsey Davenport, mtaalamu anayefanya kazi na chama cha udhibiti wa silaha, amewaambia waandishi wa Habari kwamba hali kuhusu Iran kuendelea kuimarisha mpango wake wa nyuklia ni hatari.

(DPAE, AFPE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW