Mazungumzo ya kutafuta amani Syria kufanyika mwishoni mwa mwaka
7 Novemba 2013Mjumbe huyo, Lakhdar Brahimi amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa walitegemea kutangaza tarehe rasmi ya kufanyika mkutano huo jana ingawa hawakufanya hivyo , lakini amesisitiza anataraji mkutano huo utafanyika kabla ya kumilizika mwaka huu.
Huku hayo yakiendelea wapinzani nchini Syria bado wanaonekana kugawanyika kama washiriki mkutano huo au la.
Ingawa vikao vya kupanga mazungumyo hayo vimemalizika mjini Geneva bila kufikia muafaka, hata hivyo, mjumbe huyo amesema anatarajia kukutana tena na maafisa wa Urusi na Marekani Novemba 25 mwaka huu kupanga ratiba ya majadailiano zaidi kuhusu lini mazungumzo hayo yafanyike.
Kauli ya Brahimi imefuatia mazungumzo ya viongozi wa nchi zenye nguvu zaidi duniani yanayolenga kufanikisha mazungumzo ya amani ya Syria, kufuatia mapigano yaliyodumu zaidi ya miaka miwili sasa.
Hata hivyo mjumbe huyo ameelezea wasi wasi wake kuhusu kugawanyika upande wa upinzani wa Sryia katika suala la kuhudhuria mkutano huo.
Muungano wa upinzani nchini Syria, umepanga kufanya kikao chake mjini Instanbul jumamosi wiki hiii kuamua ikiwa watahuduria mkutano huo au la, ingawa kiongozi mkuu wa upinzani ambaye ni kikwazo kikuu katika kufanikisha mazungumzo hayo ametishia kutohudhuria mkutano huo, huku makundi ya waasi yakiwatishia watakaohudhuria.
Hata hivyo, Urusi, Marekani na mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu walikubali kutuma ujumbe kwa wahusika katika mazungumzo ya kutafuta amani ya Syria.
Huku kukiwa na masuala tete juu ya mustakbal wa Rais Bashar al-Assad na iwapo mshirika wake Iran anaweza kuhudhuria mazungumzo hayo ya amani, Urusi imesisitita Iran ni lazima ihudhurie mazungumzo hayo wakati ambapo kiongozi wa upinzani Ahmed Jarba amesema muungano wake hautahudhuria kikao hicho iwapo Iran itakuwa ndani ya mazungumzo hayo.
Mwandishi: Flora Nzema/AFP
Mhariri :Hamidou Oummilkheir