Mazungumzo ya kuunda serikali Berlin yaelekea mwisho
6 Februari 2018Hali imefikia hapo baada ya kushindwa kupata muafaka wakati muda uliopangwa kufanya hivyo ukimalizika mwishoni mwa juma.
Mazungumzo baina ya chama cha Christian Democratic Union CDU , cha kansela Angela Merkel , washirika wao wa chama cha Christian Social Union CSU na kile cha SPD yamekuwa yakifanyika katika makao makuu ya chama cha DCU, baada ya kufanya mazungumzo hayo katika makao makuu ya SPD siku moja iliyopita.
Merkel alisema kabla ya kuanza tena mazungumzo hayo kwamba pande zote mbili zinahitaji kufikia maridhiano. "Kila mmoja wetu bado anahitajia kufanya maridhiano machungu. Niko tayari kufanya hivyo iwapo tutakuwa na uhakika mwishowe ambapo mambo mazuri yanashinda uzito yale ambayo si mazuri," alisema Merkel.
"Tunaweza tu kusema hatimaye kwamba kila kitu kimekubalika wakati kila kitu kitakapokubalika na bado tunahitaji kukubaliana kuhusu mada muhimu sana. Afya, sheria za kazi, kutegemewa kwetu kimataifa. Baadhi ya mambo haya yanasikika kuwa ni ya kitaalamu zaidi lakini ni kuhusiana na ubora ya maisha ya watu na kuwa na mafanikio ya kiuchumi.
Kiongozi wa chama cha SPD Martin Schulz alionesha matumaini zaidi wakati akiingia katika mazungumzo hayo. Nina sababu nzuri kufikiria tu kwamba tutamaliza leo, nina matumaini katika nia nzuri, kwa matokeo mazuri kwa ajili ya nchi yetu," Schulz alisema.
Ujerumani kuunda serikali imara
"Nafikiri kwamba leo itakuwa siku ya mwisho ambayo kutakuwa na uamuzi kuhusiana na iwapo vyama hivi vitatu , CDU/CSU na SPD vitaweza kukamilisha makubaliano ya kuunga serikali chini ya msingi ambao serikali imara ya Ujerumani itaundwa. Na si kingine zaidi ya kwamba tutaunda serikali imara katika moja ya taifa kubwa la viwanda duniani ambalo linaweza kupambana na changamoto za ndani na za kimataifa.
Vyama hivyo vimefanikiwa kufikia makubaliano katika nyanja nyingi siku ya Jumapili na Jumatatu, ikiwa ni pamoja na nyumba , malipo ya uzeeni na kuwa na mifumo ya kidigitali, lakini havikuweza kukubaliana kuhusu afya, masoko ya kazi na sera za mambo ya kigeni.
Masuala muhimu yanayorefusha mazungumzo ni madai ya chama cha SPD kufikishwa mwisho mfumo wenye ncha mbili wa afya, kupunguzwa uwezo wa makampuni kuweka masharti ya kufanyakazi na mauzo ya nje ya silaha.
Iwapo vyama hivyo vitafikia makubaliano leo, inatarajiwa vitawasilisha programu yao ya kuunda serikali na kugawana nyadhifa za serikali ifikapo kesho Jumatano licha ya kiongozi wa chama cha SPD Martin Schulz kutakiwa na wanachama kutochukua wadhifa wowote katika serikali ya Merkel kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanyiwa wanachama wa chama cha SPD.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Idd Ssessanga