Mazungumzo ya kuunda serikali yaingia hatua za mwisho
6 Februari 2018Baada ya majadiliano ya siku nzima jana Jumatatu , wajumbe wa majadiliano kutoka chama cha Angela Merkel na chama ndugu cha jimboni Bavaria cha CSU pamoja na chama kinachotarajiwa kujiunga katika serikali ya mseto cha Social Democratic SPD, vitarejea katika meza ya majadiliano mjini Berlin kwa msukumo wa mwisho kupata makubaliano kuhusu kurejea katika kile kinachofahamika kama "Muungano mkuu".
Vyama hivyo viko karibu asilimia 95 kufikia makubaliano ya kuunda serikali, amesema mjumbe wa majadiliano kutoka chama cha SPD leo, na kuongeza hatahivyo kwamba, makubaliano hayatakuwa na maana ya "kazi bora".
Licha ya vuta nikuvute iliyopo, mazungumzo hayo awali yalikuwa yamalizike mwishoni mwa juma , vyama hivyo vilionesha matumaini makubwa ya mkutano wa leo Jumanne utakuwa ni mwisho wa mazungumzo hayo.
"Bado nina matumaini ," alisema Daniel Guenther , waziri mkuu wa jimbo la kaskazini la Schleswig-Holstein kutokea chama cha CDU.
Vyanzo katika vyama hivyo vinasema maeneo yenye matatizo ni kutokubaliana kuhusu huduma za afya, sera za kazi na matumizi ya ulinzi.
Muungano wa walioshindwa
Julia Kloeckner , naibu mwenyekiti wa chama cha Merkel cha CDU, alisema anatarajia mazungumzo hayo kwa mara nyingine tena kuendelea hadi usiku wa Jumanne, ikiwa na maana yanaweza kuendelea hadi alfajiri siku ya Jumatano ili kufikiwa makubaliano ya kuunda serikali kuweza kuwasilishwa rasmi.
Merkel , ambaye yuko madarakani kwa zaidi ya miaka 12, anaweka matumaini yake ya kuongoza kwa muhula wa nne kwa kurejewa kwa muungano na chama cha SPD baada ya uchaguzi wa mwezi Septemba mwaka jana ambapo ulikiacha chama chake bila ya wingi wa kuweza kuunda serikali.
Lakini wadadisi wa masuala ya kisiasa tayari wameueleza muungano huo kuwa ni "muungano wa walioshindwa" baada ya vyama vyote kupata matokeo mabaya kuwahi kupatikana katika miongo kadhaa ya uchaguzi, wakati chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Alternative for Germany AFD kilipata asilimia 13 ya kura.
Merkel mwanzoni alitaka kuunda serikali ya muungano wa vyama vitatu na chama cha walinzi wa mazingira , Greens, na kile cha kiliberali cha FDP, lakini mazungumzo hayo yalivunjika kwa kutupiana lawama mwezi Novemba mwaka jana.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Iddi Ssessanga