Mazungumzo ya kuunda serikali Ujerumani yatatizika
29 Januari 2018Mazungumzo hayo yalianza bila ya kuonekana ukaribiano mkubwa katika masuala hayo yenye utatanishi baina ya chama cha Kansela Angela Merkel cha CDU na chama ndugu cha CSU pamoja na chama cha Social Demokratic SPD.
Chama cha SPD kinataka kujadiliwa upya suala la kuwaruhusu ndugu wa wakimbizi kuja Ujerumani kuungana na jamaa zao katika kipengele wanachokipendekeza cha ‘'Shida'' ambapo wahusika wataungana na familia zao za msingi yaani wanandoa, wazazi na watoto wao wadogo au watoto wanapokuwa hapa Ujerumani basi wazazi wao waruhusiwe kuungana nao. Chama cha SPD kinataka kanuni hiyo ijadiliwe upya kabla ya kufikia makubalino ya kuunda serikali ya mseto lakini pendekezo hilo linapingwa na vyama vya CDU na CSU.
Kiongozi wa chama cha SPD Martin Schulz amesema chama chake kinataka kuingia kwenye serikali ya muungano iliyoundwa kwa msingi madhubuti. Bunge la Ujerumani litaamua alhamisi ijayo juu ya suala la wakimbizi wanaoweza kuwaleta jamaa zao nchini Ujerumani. Bwana Schulz amesema hata hivyo vyama hivyo vimeweza kupiga hatua katika suala la kilimo.
Mjumbe wa chama cha CSU Joachim Hermann amemtaka kiongozi wa chama cha SPD Martin Schulz azingatie zaidi maslahi ya nchi badala yale ya chama chake. Bwana Hermann ambaye ni waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la Bavaria la kusini mwa Ujerumani ameliambia gazeti la Passauer Neuen Presse la hapa Ujerumani kwamba haiwezekani iwe ni upande wa vyama vya CDU na CSU tu unaokubali mengi zaidi. Chama cha CSU kinataka idadi ya wakimbizi wanaoruhusiwa nchini Ujerumani isivuke 220,000 kwa mwaka.
Mnadhimu mkuu wa ofisi ya kansela bwana Peter Altmaeir wa chama cha CDU amesema leo alfajiri baada ya vikao vya wajumbe 15 wa vyama hivyo vitatu kwamba mazungumzo yalikuwa ya makini sana. Bwana Altmaeier amesema licha ya tofauti zilizopo katika masuala ya msingi pande zote zimesisitiza kwamba zipo tayari kufikia mwafaka.
Pande zote za CDU/CSU na SPD zimekubaliana kuipa jukumu kamati maalum kulishughulikia suala hilo katika siku nzima ya leo ili kutafuta kigezo cha suluhisho.
Mwandishi:Zainab Aziz/DPA/ p.dw.com/p/2rgEI
Mhariri: Gakuba, Daniel