Mazungumzo ya kuunda serikali yaingia hatua za mwisho
4 Februari 2018Wamejiwekea muda wa mwisho kuwa leo Jumapili jioni (04.02.2018), wakiwa na fursa ya kurefusha mkutano wao hadi Jumatatu ama Jumanne. Katika ajenda ni maswali yaliyoainisha vyema juu ya vipi marudio ya kile kinachofahamika kama "Muungano Mkuu" ama kama unavyofahamika nchini kwa Kijerumani "GroKo" ambao umekuwa madarakani tangu mwaka 2013 utaelekeza huduma za afya, sheria za kazi, malipo ya uzeeni na mageuzi ya Umoja wa Ulaya na sarafu ya pamoja ya euro.
Pande zote mbili zinasita kufikia maridhiano ya kupita kiasi na kuhatarisha kupoteza uungwaji mkono, lakini pamoja na hayo pande hizo zina hofu ya kurejea kwa wapiga kura katika uchaguzi wa marudio ambao unaweza kushuhudia kupanda juu zaidi kwa kundi la siasa kali za mrengo wa kulia.
Lakini pia hakuna upande unaweza kung'ang'ania msimamo wake , wakati utafiti wa maoni uliofanywa kwa niaba ya kituo cha televisheni ya taifa cha ARD unaonesha asilimia 721 ya watu hawaelewi "kwanini uundaji wa serikali unachukua muda mrefu hivyo".
"Nina matumaini tunaweza kutimiza," Merkel amesema Ijumaa, akionya hata hivyo kwamba bado kuna "orodha nzima ya vipengee muhimu ambavyo bado hawajakubaliana".
Serikali imara
Cha muhimu kwa Merkel , ambaye bado anaonekana kuwa "anafanya vizuri" ama "vizuri sana" kwa nafasi ya ukansela ambapo asilimia 51 ya watu walioulizwa walisema katika uchunguzi huo wa maoni , ni iwapo anaongoza serikali imara ya muungano katika muhula wake wa nne wa uongozi, ama anahatai ya kuingia katika serikali tete isiyo na wingi ama kurejea katika uchaguzi mpya.
Chama cha SPD ni mshirika wa shingo upande, baada ya hapo kabla kuapa kuingia katika upinzani baada ya kupata matokeo ya chini katika historia ya chama hicho ya asilimia 20.5 katika uchaguzi wa mwezi Septemba.
Wanachama wa Social Democrat walikubali kuingia katika mazungumzo pale tu kushindwa kukubaliana na vyama vidogo , chama cha walinzi wa mazingira , cha kijani na kile kinachopendelea biashara cha Free Democratic FDP.
Akipata changamoto kutoka kwa waasi katika chama chake, kiongozi wa SPD Martin Schulz aliona bora kupata ulinzi wa kisiasa kwa kupeleka makubaliano ya mwisho ya kuunda serikali ya mseto katika kura ambapo wanachama 440,000 watapiga kura kukubali ama kukataa.
Tawi la vijana
Kevin Kuehnert , kiongozi wa tawi la vijana la chama cha SPD , amekuwa mshika bendera ya upinzani wa makubaliano mapya na Merkel.
"Aina hii ya siasa ilizawadiwa na upungufu wa asilimia 14 kwa CDU na SPD kwa jumla mwaka jana, na nina shaka mambo yataendelea hivi hivi "iwapo muungano wa serikali utafanikiwa, alisema.
Wengine wanaonya SPD iko dhaifu sana kuwakabili wapiga kura kwa mara nyingine tena haraka, ikipata asilimia 18 katika baadhi ya uchunguzi wa maoni ya wapiga kura, kiasi ya pointi chache mbele ya chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Alternative for Germany, chama mbadala kwa Ujerumani AfD.
Merkel pia anakabiliwa na manung'uniko miongoni mwa wanachama wake, kukiwa na sauti zinazopazwa za wahafidhina zikimshutumu kwa kukipeleka chama chake cha Christian Democratic Union CDU kuelekea zaidi siasa za wastani , na kutoa fursa kwa chama cha AfD.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Yusra, Buwayhid