1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya mpango wa nyuklia wa Iran yaahirishwa

Zainab Aziz Mhariri: Rashid Chilumba
2 Mei 2021

Duru ya tatu ya mazungumzo na Iran juu mpango wake wa nyuklia yaliyokuwa yanafanyika mjini Vienna, Austria yameahirishwa. Wajumbe wa Ulaya waelezea wasiwasi wao juu ya kujikongoja kwa mazungumzo hayo.

Österreich | Treffen zum iranischen Atomabkommen in Wien
Picha: EU Delegation in Vienna/REUTERS

Duru ya tatu ya mazungumzo na Iran juu mpango wake wa nyuklia yaliyokuwa yanafanyika mjini Vienna, Austria yaliahirishwa hapo siku ya Jumamosi. Lengo la mazungumzo hayo ni kuirudisha Marekani katika makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa makubwa sita.

Wajumbe wa Ujerumani, Ufaransa na Uingereza ambayo ni mataifa yaliyo sehemu ya mkataba huo wa nyuklia wamesema licha ya kwamba kila upande umeonesha utayarifu wa kuurejesha mkataba huo uliotiwa saini mwaka 2015, hatua zilizopigwa hadi sasa hazijafika mbali.

Soma Zaidi: Iran yaonya hujuma zinaathiri mazungumzo ya Vienna 

Tangu mwanazoni mwa mwezi Aprili wanadiplomasia hao pamoja na wengine kutoka China na Urusi wanakutana mjini Vienna kwa mazungumzo ya kujaribu kuishawishi Marekani kurejea kwenye mkataba wa nyuklia na Iran baada ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Donald Trump kuiondoa nchi yake kutoka kwenye mkataba huo mnamo mwaka 2018.

Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Andrew Harnik/AFP/Getty Images

Iran ambayo pia inashinikizwa kuheshimu masharti ya mkataba huo imesema bado kuna tofauti kubwa kuhusu masuala muhimu lakini itaendelea kushiriki kwenye duru nyingine ya mazungumzo wiki ijayo.

Kwa upande wake Urusi imeonesha kuwa na tahadhari lakini wakati huo huo imeeleza juu ya kuongezeka kwa matumaini huku ikisema matokeo madhubuti huenda yakapatikana katika muda wa wiki tatu lakini chanzo cha kidiplomasia kutoka upande wa nchi tatu za Ulaya ambazo ni Ujerumani, Ufaransa na Uingereza kimesema bado hawajaafikiana juu ya mambo muhimu zaidi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi anayeongoza ujumbe wa Iran amesema mazungumzo hayo yamefikia mahala pa kutia moyo ingawa hatua zaidi zinahitajika. Araghchi ametaka vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa dhidi ya Iran viondolewe. Iran imewekewa vikwazo katika sekta za nishati, fedha, viwanda vya magari, mabenki, bima na maswala ya bandari.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas AraghchiPicha: Leonhard Foeger/REUTERS

Baada ya Donald Trump kuiondoa Marekani kwenye mkataba huo, pande nyingine zilizotia saini mktaba huo wa mwaka 2015 zimekuwa zinaendelea na mazungumzo tangu mwezi April kwa lengo la kuurejesha mkataba huo.

Soma Zaidi: Hofu yazuka baada ya Iran kurutubisha madini ya urani

Rais wa Marekani Joe Biden anaunga mkono mkataba huo wa nyuklia ambao Iran ilikuwa inautekeleza kabla ya Trump kuiwekea vikwazo nchi hiyo. Biden ameitaka Iran iache mipango yake ya kurutubisha madini ya Urani kabla ya Marekani kuiondolea vikwazo. 

Hata hivyo Iran mpaka sasa imekataa kukutana ana kwa ana na Marekani na badala yake wajumbe wa nchi nyingine zilizotia saini mkataba na Iran ambao ni nchi za Ulaya, Urusi na China walikutana na wajumbe wa Marekani Jumamosi asubuhi. Mazungumzo hayo yaliyoahirishwa yataendelea wiki ijayo.

Vyanzo:DPA/AFP

 

  

  

     

  

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW