1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIran

Mazungumzo ya Marekani na Iran yaisha bila makubaliano

27 Februari 2026

Iran na Marekani zimefanya mazungumzo marefu mjini Geneva kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran bila kufikia makubaliano, huku hofu ya vita vya kikanda ikiongezeka kutokana na ongezeko kubwa la majeshi ya Marekani.

Uswisi, Geneva 2026 | Wajumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff na Jared Kushner katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kuhusu Iran mjini Geneva.
Jared Kushner, Steve Witkoff na Badr Al-Busaidi (kutoka kushoto kwenda kulia kwenye picha) walipokutana mjini Geneva mapema Alhamisi.Picha: Omani Foreign Ministry/AFP

Mazungumzo ya saa kadhaa kati ya Iran na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran yamekamilika mjini Geneva bila makubaliano ya mwisho. Hata hivyo, wapatanishi wamesema kulikuwa na maendeleo muhimu katika mazungumzo hayo. Kutokuwepo kwa makubaliano kumeacha hatari ya mzozo wa kijeshi ikiendelea kutanda katika eneo la Mashariki ya Kati.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr Albusaidi, ambaye alisimamia mazungumzo hayo, alisema kulikuwa na "maendeleo makubwa” bila kufafanua vipengele vilivyokubaliwa. Oman imeendelea kuwa mpatanishi muhimu kati ya Tehran na Washington kwa miaka mingi. Kauli yake imeongeza matumaini kuwa njia ya diplomasia bado ipo wazi.

Hata hivyo, kabla ya kumalizika kwa mazungumzo hayo, vyombo vya habari vya serikali ya Iran viliripoti kuwa Tehran itaendelea kurutubisha urani. Iran imekataa pendekezo la kuhamisha urani yake nje ya nchi na kusisitiza kuondolewa kwa vikwazo vya kimataifa. Hali hiyo inaonyesha kuwa bado kuna tofauti kubwa kati ya pande hizo mbili.

Rais wa Marekani, Donald Trump, anataka makubaliano yatakayodhibiti kabisa mpango wa nyuklia wa Iran. Pia amesisitiza kuwa Iran inapaswa kujadili mpango wake wa makombora ya masafa marefu na msaada wake kwa makundi yenye silaha katika eneo hilo. Kwa upande wake, Iran inasema iko tayari kujadili nyuklia pekee.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alieleza kuwa mazungumzo hayo yalikuwa miongoni mwa yaliyo makali na marefu zaidi kuwahi kufanyika. Alisema baadhi ya masuala yamepata mwafaka huku mengine yakiendelea kuwa na tofauti. Hata hivyo, hakutoa maelezo ya kina kuhusu vipengele vilivyokubaliwa.

Maafisa wa polisi walilinda nje ya makazi ya balozi baada ya waandamanaji wa Iran kulenga mazungumzo ya wiki iliyopita.Picha: Martial Trezzini/KEYSTONE/picture alliance

Mazungumzo ya kiufundi kufanyika Vienna

Albusaidi alitangaza kuwa mazungumzo ya kiufundi yatafanyika wiki ijayo mjini Vienna. Majadiliano hayo yatahusisha wawakilishi wa ngazi ya chini pamoja na wataalamu wa nyuklia. Vienna ni makao ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Nyuklia, IAEA, taasisi yenye jukumu la kusimamia shughuli za nyuklia duniani.

Wakala huo wa Umoja wa Mataifa unatarajiwa kuwa kiungo muhimu katika kusimamia utekelezaji wa makubaliano yoyote yatakayofikiwa. Bila ushiriki wake, itakuwa vigumu kuhakikisha uwazi na ufuatiliaji wa shughuli za nyuklia za Iran. Hivyo, mazungumzo ya kiufundi yanaonekana kuwa hatua muhimu kuelekea makubaliano mapya.

Wakati huo huo, hakuna kauli rasmi iliyotolewa mara moja na Ikulu ya Marekani kuhusu matokeo ya mazungumzo hayo. Hata hivyo, duru za habari zimenukuu maafisa wa Marekani wakisema mazungumzo yalikuwa "chanya.” Hali hiyo inaashiria kuwa mlango wa mazungumzo bado haujafungwa.

Mazungumzo haya yanafanyika wakati Marekani imelundika meli za kivita, ndege za kivita na manowari katika eneo la Ghuba. Hatua hiyo imezua hofu ya uwezekano wa mashambulizi ya kijeshi iwapo diplomasia itashindwa. Iran imeonya kuwa mashambulizi yoyote yataleta majibu makali.

Iwapo Marekani itachukua hatua ya kijeshi, Iran imesema kambi za kijeshi za Marekani katika eneo hilo zitakuwa shabaha halali. Hilo linaweza kuhatarisha maisha ya maelfu ya wanajeshi wa Marekani walioko Mashariki ya Kati. Aidha, Iran imeonya kuwa Israel pia inaweza kulengwa iwapo itahusika.

Iran inavyoweza kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Marekani

01:42

This browser does not support the video element.

Hofu ya vita vya kikanda

Araghchi alihoji kuwa vita havitaleta ushindi kwa upande wowote. Alisema mzozo wa kijeshi unaweza kuhusisha eneo lote kutokana na uwepo wa kambi za Marekani katika nchi mbalimbali. Kauli yake imeongeza uzito wa tahadhari kuhusu madhara ya mzozo huo.

Mtaalamu wa masuala ya Iran, Ali Vaez kutoka shirila ufuatiliaji wa mizozo ya kimataifa, International Crisis Group, amesema ni ishara nzuri kuwa Marekani haikuondoka mezani mara moja. Kwa mujibu wake, uwepo wa mazungumzo unaonyesha kuna msingi fulani wa makubaliano. Hata hivyo, alionya kuwa kufikia makubaliano kamili bado ni safari ndefu.

Mazungumzo ya Geneva ni ya tatu tangu vita vya Juni vilivyodumu kwa siku 12 kati ya Israel na Iran. Wakati huo, Marekani iliungana kwa muda mfupi na Israel kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran. Mashambulizi hayo yaliathiri kwa kiasi kikubwa miundombinu ya nyuklia ya Tehran.

Marekani inataka Iran kusitisha kabisa urutubishaji wa urani. Iran, hata hivyo, inasisitiza kuwa mpango wake ni wa amani na kwa matumizi ya kiraia pekee. Pia inadai kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi vinavyoathiri uchumi wake vibaya.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, Iran bado inajaribu kujenga upya baadhi ya vipengele vya mpango wake wa nyuklia. Hata hivyo, Iran imesema haijarutubisha urani tangu Juni mwaka jana. Ukosefu wa uwazi umeendelea kuzua maswali kimataifa.

Marekani imeendelea kuweka zana za kivita karibu karibu na Iran, licha ya kusema kwamba inaamini zaidi katika diplomasia kutatua mvutano na taifa hilo.Picha: Christian Kibler/US Navy/AFP

Shinikizo la kisiasa na kijeshi

Trump ametoa muda wa siku 10 hadi 15 kwa Iran kufikia makubaliano. Amesema iwapo hilo halitatokea, "mambo mabaya sana” yanaweza kutokea. Kauli hiyo imeongeza shinikizo katika mazungumzo yanayoendelea.

Ndani ya Iran, Kiongozi Mkuu Ali Khamenei anakabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi na kisiasa. Uchumi wa nchi hiyo umedorora kutokana na vikwazo na maandamano ya mara kwa mara. Serikali inalazimika kusawazisha kati ya msimamo mkali na hitaji la kupunguza shinikizo la ndani.

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema fatwa ya kidini inakataza utengenezaji wa silaha za maangamizi makubwa. Kauli hiyo inalenga kuondoa hofu kuwa Iran inakusudia kutengeneza bomu la nyuklia. Hata hivyo, nchi za Magharibi bado zina wasiwasi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesisitiza kuunga mkono njia ya diplomasia. London imeripotiwa kusita kuruhusu matumizi ya kambi ya Diego Garcia kwa mashambulizi dhidi ya Iran. Hatua hiyo inaonyesha mgawanyiko wa kimkakati miongoni mwa washirika wa Magharibi.

Kwa sasa, macho ya dunia yanaelekezwa Vienna ambako mazungumzo ya kiufundi yatafanyika. Hatma ya makubaliano mapya inaweza kuamua iwapo eneo la Mashariki ya Kati litaingia katika vita vingine au la. Diplomasia imepewa nafasi ya mwisho kabla ya hatari ya mzozo mkubwa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW