1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya nyuklia na Iran kuendelea Vienna

Josephat Charo
8 Februari 2022

Mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yanatarajiwa kuendelea tena Jumanne (08.02.2022) mjini Vienna, Austria baada ya kusitishwa mwishoni mwa mwezi Januari.

Österreich Wien JCPOA-Gespräche Iran | Hotel Palais Coburg
Picha: Alex Halada/AFP/Getty Images

Marekani imesema inawezekana mkataba ukapatikana na Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia lakini makubaliano yanatakiwa kukamilishwa haraka huku serikali ya mjini Tehran ikiimarisha uwezo na shughuli zake za nyuklia. Mazungumzo ya mjini Vienna yanayohudhuriwa na China, Ufaransa, Ujerumani, Urusi, Uingereza na Marekani yanarejea tena baada ya kusitishwa mwezi uliopita na yanafanyika baada ya pande husika kuzungumzia kupatikana kwa mafanikio katika kuufufua mkataba wa mwaka 2015 ulionuiwa kuizuia Iran kutengeneza na kumiliki bomu la nyuklia, lengo ambalo Iran yenyewe imekuwa ikilikanusha.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani amesema mkataba unaoshughulikia masuala yote ya msingi ya pande zote husika unakaribia kuafikiwa, lakini kama hakutapatikana makubaliano katika wiki zijazo, shughuli za Iran kujiimarisha zitaifanya vigumu kurejea kwenye mkataba wa mwaka 2015. Mazungumzo ya pande sita yamekuwa yakiendelea mjini Vienna tangu mwaka uliopita huku Marekani ikishiriki ingawa sio moja kwa moja.

Iran ilisema jana kwamba Marekani inatakiwa kufanya maamuzi ya kisiasa kuhusu kuiondolea vikwazo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikisema masharti ya serikali ya mjini Tehran kutaka vikwazo hivyo viondolewe kikamilifu ili kuufuua mkataba wa mwaka 2015 hayana mjadala.

Makubaliano yatategemea msimamo wa Marekani

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Saeed Khatibzadeh amesema muda unaohitajika kufikia makubaliano utategemea masuala mawili muhimu - Majibu ya Marekani kwa maswali yaliyoulizwa na vipengee kuhusu kulegezwa vikwazo na kasi ya upande unaopinga katika meza ya mazungumzo. "Leo ni fursa kwa Marekani kuja Vienna na ajenda iliyo wazi badala ya lawama na hatua zisizosaidia kuthibitisha mabadiliko ya tabia. Wakija na ajenda iliyo wazi na maamuzi ya kisiasa kuhusu kufuta vikwazo na kutimiza ahadi zao, bila shaka inawezekana kufikia makubaliano katika muda mfupi."

Ali Bagheri, mjumbe maalumu wa Iran katika mazungumzo ya nyukliaPicha: Guo Chen/Xinhua/picture alliance

Msemaji huyo wa wizara ya mambo ya nje ya Iran amethibiisha kwamba mjumbe mkuu maalumu wa nchi hiyo anayeshughulikia masuala ya nyuklia, Ali Bagheri, atahudhuria mazungumzo ya Vienna.

Baada ya miezi minane ya mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati ya Iran na Marekani tangu mwezi Aprili mwaka uliopita, tofauti zingalipo kuhusu kasi na upana wa kufuta vikwazo dhidi ya Iran, yakiwemo matakwa ya Iran kutaka hakikisho la Marekani kutopitisha hatua zaidi za kuiadhibu, na jinsi na wakati gani wa kurejesha vikwazo kuhusiana na shughuli za nyuklia za Iran.

Mazungumzo ya Vienna yalisita Januari 28 wakati wapatanishi wakuu waliporejea nchini kwao kwa mashauriano. Mjumbe maalumu wa Mareakni kwa ajili ya Iran Robert Malley alisema Jumapili iliyopita kwamba angerejea Vienna hivi karibuni, akisisitiza mkataba ungeweza kufufuliwa.

Utawala wa rais wa Marekani Joe Biden siku ya Ijumaa ulirejesha msamaha wa vikwazo kwa Iran kuruhusu miradi ya ushirikiano wa kimataifa ya nyuklia huku mazungumzo kuhusu mkataba wa nyuklia mwaka 2015 kati ya Marekani na Iran yakiingia awamu ya mwisho. Marekani imetaka mazungumzo ya ana kwa ana lakini yanaendelea kufanyika kwa njia isiyo ya moja kwa moja kufuatia ombi la Iran.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameyaita mazungumzo hayo kuwa wakati muhimu wa maamuzi katika mahojiano na gazeti la Washington yaliyochapishwa Jumatatu.

afp

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW