1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Mazungumzo ya uanachama wa Ukraine EU yapendekezwa Brussels

8 Novemba 2023

Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya imependekeza kufungua mchakato wa majadiliano ya Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya iwapo itatimiza masharti iliyowekewa licha ya changamoto inazopitia katika vita vyake na Urusi.

Rais wa Halmashauri Kuu wa Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen
Rais wa Halmashauri Kuu wa Umoja wa Ulaya Ursula von der LeyenPicha: Yves Herman/REUTERS

Halmashauri hiyo kuu ya Umoja wa Ulaya, imesema mabadiliko katika vita vya Ukraine dhidi ya ufisadi na umuhimu wa kuzuwia zaidi ushawishi wa matajiri wa Urusi nchini humo, pamoja na ulinzi wa maeneo yanayokaliwa na wachache ni lazima yatimizwe kabla ya duru ya kwanza ya mazungumzo kuanza.

Akizungumza mjini Brussels, Rais wa Halmashauri hiyo Ursula Von der Leyen amesema Ukraine inaendelea kupitia changamoto chungu nzima zinazochangiwa na uvamizi wa Urusi katika taifa hilo. lakini akasema licha ya hilo bado waukraine wanaendelea kufanya mabadiliko makubwa nchini mwao.

Umoja wa Ulaya watafakari uanachama wa Ukraine

Ukraine pamoja na jirani yake Moldova waliomba kujiunga na Umoja wa Ulaya mapema mwaka 2022, muda ambao Urusi ilimvamia kikamilifu jirani yake huyo na baadae mwezi Juni zikatajwa kuwa wagombea rasmi wa nafasi hiyo.

Wakati huo Kiev ilipewa orodha ya mabadiliko ya kuyatekeleza katika maeneo saba muhimu yaliyohitaji kufanikishwa kabla ya mazungumzo rasmi ya kujiunga na Umoja huo kuanza.

Zelensky ataka majadiliano ya Ukraine kujiunga na EU yaanze

Maeneo hayo ni pamoja na mchakato wa kuwateua majaji wa mahakama ya kikatiba, wanachama wa Baraza la juu la kisheria, vita dhidi ya utakatishaji fedha, kuzuwia ushawishi wa matajiri wa Urusi na uhuru wa vyombo vya habari.

Zelensky ausifia uamuzi wa Halamashauri kuu ya Umoja wa Ulaya

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akiwa na Rais wa Halmashauri Kuu wa Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen mjini Kiev, UkrainePicha: Sergei Supinsky/AFP/Getty Images

Rais wa Ukraine Vladimir Zelensky ameusifia uamuzi huo aliouita wa kihistoria kwa taifa lake kupendekezwa na Halmashauri  kuu ya Umoja wa Ulaya kualikwa  katika majadiliano ya taifa lake kujiunga na umoja wa Ulaya, iwapo itakamilisha matakwa yanayohitajika licha yakuwa vitani na Urusi.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kuamua kuhusu kuanza kwa mchakato huo katika mkutano wao wa Desemba, kwa kuzingatia ripoti ya leo. (08.11.2023) Majadiliano hayo hata hivyo huenda yakachukua miaka kadhaa  na hakuna hakikisho lolote la moja kwa moja kwamba mataifa hayo mawili, Ukraine na Moldova yatajiunga na Umoja huo.

Zelensky hayuko tayari kuzungumza na Urusi

Ripoti inayohusu Ukraine ni sehemu ya tathimini ya ripoti ya Halmashauri hiyo kufuatilia mchakato wa mabadiliko yanayofanywa na mataifa yote 10 yanayonuia kujiunga na Umoja wa Ulaya ikiwemo Moldova, Georgia na baadhi ya mataifa ya Magharibi mwa Balkan.  Kulingana na tathimini ya Halmashauri hiyo, Georgia inapaswa kutajwa kama mgombea rasmi wa EU ikiwa ndio hatua ya kwanza ya safari ya kujiunga na Umoja huo.

Putin: Silaha za msaada za Ukraine zinauzwa kwa Taliban

Rais wa taifa hilo Salome Zurabishvili ameipongeza hatua hiyo na kusema anafurahjia pamoja na watu wa Georgia huku akiwahimiza kukusanyika pamoja kwa maandamano ya kuiunga mkono Umoja wa Ulaya na kusema kwa mara nyengine tena kwamba siku zao za usoni haziko pamoja na Urusi.

Mwaka mmoja tangu Urusi kuivamia Ukraine

01:51

This browser does not support the video element.

Vyanzo: dpa/reuters/ap/afp

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW