Muda wayoyoma kwa mazungumzo ya Ugiriki
12 Julai 2015Mazungumzo ya mawaziri wa fedha ya kanda ya sarafu ya euro yalisitishwa usiku wa manane hapo Jumamosi baada ya majadliano ya masaa tisa kushindwa kufikia makubaliano. Mawaziri wa fedha wa nchi wanachama 19 wa kundi la nchi zinazotumia sarafu ya euro zina masaa machache kufikia msimamo kabla ya kuanza kwa mkutano wa kilele wa viongozi wa kanda ya sarafu euro Jumapili.
Mkutano wa Kilele wa nchi zote wanachama 28 wa Umoja wa Ulaya uliokuwa umepengwa kufanyika Jumapili jioni hivi sasa umefutwa na Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk.
Katika ujumbe kupitia mtandao wa Twitter Tusk amesema mkutano wa viongozi wa kanda ya sarafu ya euro utaendelea hadi hapo mazungumzo kuhusu Ugiriki yatakapokuwa yamehitimishwa.
Mazungumzo magumu sana
Mkuu wa kundi la sarafu ya euro Jeroen Dijsselboem amewaambia waandishi wa habari mjini Brussels kwamba wameshindwa kukamilisha mazungumzo yao na kuongeza kwamba mazungumzo bado ni magumu sana lakini wanapiga hatua.
Waziri wa Fedha wa Ugiriki Euclid Tsakalotos anatakiwa kushawishi wakopeshaji wa kimataifa kwa nchi yake yaani Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Benki Kuu ya Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF kwamba nchi yake itatimiza ahadi zake kutekeleza mageuzi mapya magumu ili iweze kupatiwa msaada wa mkopo wa mabilioni ya euro kuinusuru isifilisike na madeni.
Hatua zilizopendekezwa na Ugiriki zinazojumuisha mageuzi makubwa ya mfumo wa malipo ya wastaafu, kupandisha kodi na ubinafsishaji ziliidhinishwa na bunge la nchi hiyo hapo Jumamosi na pia kuungwa mkono kwa tahadhari na wakopeshaji.
Suala la uaminifu
Mawaziri kadhaa wa fedha waliokutana Brussels wameelezea wasi wasi wao kutokana na ukosefu wa kitu cha maana katika mapendekezo hayo yaliowasilishwa na Ugiriki na iwapo nchi hiyo yenye ukata wa fedha inaweza kuaminika kwamba itatekeleza mageuzi hayo.
Dijesselboem amesema baada ya kuahirishwa kwa mkutano wao hapo Jumamosi kwamba wamekuwa na mazungumzo ya kina juu ya mapendekezo hayo ya Ugiriki na kwamba suala la uaminifu limejadiliwa pamoja na masuala ya fedha yanayohusika nayo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Uingereza Reuters mawaziri hao wametaka serikali ya Ugiriki ijitolee zaidi katika suala la kufunguwa zaidi soko la bidhaa, kuregeza sheria za ajira, uwekezaji,mageuzi katika taasisi za serikali na kupunguza matumizi ya ulinzi.
Duru zilio karibu na mazungumzo hayo zimeliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwamba zaidi ya nchi 10 kati ya 19 za kanda ya sarafu ya euro zimekuwa na wasi wasi mkubwa kuhusiana na masuala hayo wakati Ufaransa na mataifa mengine machache yameunga mkono mpango huo wa Ugiriki.
Matumaini yameangamizwa
Waziri wa fedha wa Ujerumani mwenye msimamo mkali Wolfgang Schäuble amesema kanda ya sarafu ya euro haiwezi kuitegemea Ugiriki kutimiza ahadi zake.Amesema katika miezi iliopita matumaini yaliangamizwa vibaya na kwamba wameazimia kutofanya mahesabu ambayo kila mtu anajuwa kwamba hakuna atakayoamini.
Wizara ya Fedha ya Ujerumani hapo Jumamosi ilitowa waraka wa msimamo wake ukikosoa mapendekezo mapya ya Ugiriki na kuitaka Ugiriki aidha irekebishe mpango wake wa mageuzi ili kuweza kupatiwa mkopo wa uokozi au ipumzike kwa miaka mitano kwa kujitowa kwenye kanda ya sarafu yya euro na kurekebisha deni lake.
Ugiriki imewataka wakopeshaji wake iwapatie msaada wa mkopo wa uokozi kuinusuru isifilisike wa euro bilioni 53.5 na kuizuwiya isitoke kwenye kanda ya sarafu ya euro. Ugiriki tayari ilikuwa imepatiwa euro bilioni 240 katika mikopo miwili ya uokozi iliopita katika kipindi cha miaka mitano iliopita.
Iwapo nchi hiyo itashindwa kupatiwa fedha zaidi kutoka kwa wakopeshaji nchi hiyo inaweza kuachiliwa ifilisike na kutoka kwenye kanda ya sarafu ya euro.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/AFP/Reuters,dpa
Mhariri : Bruce Amani