1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Urusi, Ukraine yapiga hatua kidogo

8 Machi 2022

Wajumbe wa timu za mazungumzo ya kusitisha mapigano kutoka Urusi na Ukraine wanaripoti kupigwa kwa hatua japo ndogo kwenye duru ya mazungumzo hayo yaliyofanyika nchini Belarus, huku Urusi ikitangaza njia salama kwa raia.

Ukraine-Konflikt | Evakuierung von Zivilisten | Stadt Irpin in der Nähe von Kiew
Picha: Andrea Filigheddu/NurPhoto/picture alliance

Duru hiyo ya tatu ya mazungumzo baina ya Urusi na Ukraine ilimalizika jioni ya Jumatatu (Machi 7), huku afisa mmoja wa ngazi za juu wa Ukraine akisema kumepatikana maendeleo madogo ambayo hakuyataja, kuelekea kuanzishwa kwa njia salama zitakazowawezesha raia kukimbia mapigano, ambapo mkuu wa timu ya Urusi kwenye mazungumzo hayo alisema anatazamia njia hizo zingelianza kufunguliwa Jumanne. 

Hata kabla ya kutekelezwa kwa makubaliano hayo, tayari Urusi ilishasema ingeliruhusu raia kuondoka kwenye miji ya Ukraine, ukiwemo mji mkuu, Kyiv, kuanzia saa 3:00 asubuhi ya Jumanne (8 Machi) kwa mujibu wa mashirika ya habari ya Urusi. Hata hivyo, nyingi ya njia hizo zingelikuwa zinapitia Urusi na Belarus, jambo ambalo mamlaka nchini Ukraine ililikataa. 

Shirika la habari la Interfax lilimnukuu afisa mmoja wa ngazi ya juu anayehusika na njia hizo, akisema kwamba raia wanaoondoka miji ya Kyiv, Chernigov na Kharkiv wangelielekea Urusi wakipitia Belarus. Hata hivyo, watu wanaoondoka kwenye mji wa Sumy na Mariupol wangelipewa fursa ya kuchaguwa ama kupitia Urusi ama miji ya Ukraine ya Potlava na Zaporizhia, kwa mujibu wa wafisa huyo. 

Urusi yatowa muda maalum kwa Ukraine

Watu wakivuuka daraja lililobomolewa wakati wakikimbia mji wa Irpin ulio karibu na Kyiv Jumatatu ya 7 Machi 2022.Picha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance

Urusi iliipa Ukraine hadi saa tisa ya usiku wa kuamkia Jumanne kuamuwa endapo inakubaliana na masharti ya kuwekwa njia hizo za kuwaokowa raia, lakini tayari Rais Volodymyr Zelenskiy alilikataa pendekezo hilo la kuwahamisha raia wa nchi yake kupitia kile anachokiita "ardhi ya mvamizi". 

Zelenskiy alisema badala ya kutangaza makubaliano ya kuwepo kwa njia salama, "Urusi inaongeza vifaru, makombora na mabomu."  Akizungumza akiwa ofisini mwake mjini Kyiv, Zelensky aliapa kuendelea kubakia ndani ya nchi kuongoza mapambano.

Mapema, balozi wa Ukraine kwenye Umoja wa Mataifa, Sergiy Kyslytsya, aliuambia mkutano wa Baraza la Usalama kwamba Urusi ilikuwa inahujumu mipango ya kuwepo njia za salama za kupitia raia kwa kusisitiza kwamba njia zote zielekee Urusi ama Belarus.

Ama ikiwa makubaliano yaliyopatikana kwenye duru ya tatu ya mazungumzo yatatelekezwa kikamilifu, bado ni suala la kungoja na kuona, ikizingatiwa kwamba majaribio ya awali ya kuwaondosha raia kupitia njia salama yalishindwa, kutokana na mapigano makali. 

Hali mbaya ya kibinaadamu 

Sehemu ya jengo lililovunjwa kwa mashambulizi nchin Ukraine.Picha: Emilio Morenatti/AP Photo/picture alliance

Kwenye mji wa Mariupol wenye wakaazi 430,000, ambako wanajeshi wa Urusi walikuwa wanasonga mbele, raia 200,000 walitazamiwa kuukimbia mji huo siku ya Jumanne, huku maafisa wa Msalaba Mwekundu wakingojea kuona endapo njia za salama zingelifunguliwa.

Mji huo unaripotiwa kuwa na upungufu mkubwa wa maji, chakula na umeme, huku mitandao ya simu za mkononi ikipatikana kwa shida. Maduka yameporwa wakati wakaazi wakisaka bidhaa muhimu.

Katika mji mkuu, Kyiv, wanajeshi na wafanyakazi wa kujitolea wamejenga vizuizi kadhaa vya barabarani kuulinda mji huo wenye wakaazi wapatano milioni nne, wakitumia magunia ya michana, matairi na nyaya. Meya Vitali Klitschko amesema kila nyumba, kila mtaa, na kila kizuizi cha barabarani kitapambana hadi mwisho ikibidi. 

Juhudi za kimataifa zaendelea

Mabalozi wa Uingereza na Marekani wakihudhuria kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine tarehe 7 Machi 2022.Picha: Carlo Allegri/REUTERS

Katika upande wa kimataifa, bado mataifa yenye nguvu yalikuwa yanajadiliana uwezekano wa kuipa ndege za kijeshi Ukraine kama ambavyo limekuwa ombi la muda mrefu la Rais Zelensky, kwa mujibu wa afisa mmoja wa ngazi za juu wa Marekani.

Siku ya Jumanne, Benki ya Dunia ilisema bodi yake ya wakurugenzi imeidhinisha kitita cha dola milioni 723 kinachohusisha mikopo na misaada kwa Ukraine, ikiunga mkono bajeti ya taifa hilo linalokabiliana na uvamizi wa Urusi.

Fedha hizo zinajumuisha dola milioni 350 kama nyongeza ya mkopo wa awali wa Benki ya Dunia, zikipatikana kupitia dhamana za Uholanzi na Sweden.

Taarifa ya benki hiyo iliyotolewa jana inasema kwamba fedha hizo zinajumuisha pia dola milioni 134 za msaada kutoka Uingereza, Denmark, Latvia, Lithuania na Iceland, na pia ufadhili wa dola milioni 100 kutoka Japan. 

Kinu cha nyuklia Kharkiv chaathirika

Picha: Dominic McGrath/PA/picture alliance

Shirika la Nishati ya Nyuklia la Umoja wa Mataifa (IAEA) lilisema kuwa limepokea taarifa kutoka serikali ya Ukraibe kwamba kituo chake kipya ya utafiti wa mionzi ya nyuklia kwa ajili ya matibabu na matumizi ya viwandani kimeathiriwa kwa mashambulizi mjini Kharkiv.

Hata hivyo, IAEA ilisema mashambulizi ya siku ya Jumapili (Machi 6) dhidi ya kituo hicho, hayakuongeza kiwango cha mionzi. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nishati ya nyuklia kwenye kituo hicho ipo kwenye kiwango ambacho hakiwezi kuleza madhara makubwa ya mionzi, kama ilivyokhofiwa awali.

Shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Vienna, Austria, imeelezea wasiwasi wake juu ya usalama wa vinu vya nyuklia ndani ya Ukraine, wakati huu wa uvamizi wa Urusi.

Siku ya Jumatatu, IAEA ilitowa taarifa nyengine juu ya hatima ya kinu chengine cha nyuklia cha Zaporizhzhia, ambacho ndicho kikubwa kabisa nchini Ukraine, na ambacho kimeangukia mikononi mwa jeshi la Urusi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW