1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kuutatua mzozo wa Gaza zaendelea Doha

Angela Mdungu
16 Agosti 2024

Juhudi za kimataifa za kuzuia vita kati ya Israel na kundi la Hamas visiwe mzozo wa Kikanda, zinaendelea wakati wasuluhishi wa kimataifa wakiingia katika siku ya pili ya mazungumzo mjini Doha nchini Qatar.

Wapalestina katika mji wa Khan Younis Julai 30.2024
Wakaazi wa Gaza wasio na makazi kutokana na mashambulizi ya Israel Picha: Mohammed Salem/REUTERS

Hayo yanajiri wakati Israel ikikabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa raia wake walioandamana mjini Tel Aviv, wakiishinikiza serikali ifikie makubaliano yatakayowarejesha nyumbani mateka haraka iwezekanavyo.

Wapatanishi hao wa kimataifa wanaendelea kutafuta suluhisho la mzozo wa Gaza wakati mawaziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza na Ufaransa wakielekea Israel wanakotarajiwa kusisitiza umuhimu wa kuepuka vita kubwa zaidi haraka iwezekanavyo.

Wanafanya safari hiyo huku mazungumzo ya usuluhishi yakiendelea Qatar bila ya uwepo wa kundi la Hamas lililoituhumu Israel kwa kukwamisha makubaliano. Kundi hilo linasisitiza kuwa halitaki makubaliano mapya bali masharti ya makubaliano ya awali yanapaswa kutekelezwa.

Soma zaidiDuru mpya ya mazungumzo kuhusu mzozo wa Gaza

Msukumo mpya wa kuvimaliza vita kati ya Israel na kundi la Hamas umeibuka wakati idadi ya vifo vya Wapalestina kwenye Ukanda wa Gaza ikiwa imeshazidi watu 40,000 kwa mujibu wa mamlaka za afya za Gaza zilizo chini ya Hamas.

Idadi hiyo inazidi kuongezeka wakati hofu ikiendelea kutanda kuwa huenda Iran na wanamgambo wa Hezbollah wa nchini Lebanon wakaishambulia Israel kama hatua ya kulipa kisasi baada ya kuuwawa kwa viongozi wawili wa juu.

Matumaini mapya ya kupatikana kwa suluhisho

Msemaji wa baraza la Usalama la Marekani John Kirby amesema awamu ya sasa ya mazungumzo imeanza vyema ingawa ameeleza pia kuwa bado kuna kazi kubwa inayohitaji kufanyika.

Wakati hayo yakiendelea, serikali ya Israel inakabiliwa pia na shinikizo kubwa ndani ya nchi hiyo. Maelfu ya raia wake waliandamana Alhamisi jioni mjini TelAviv wakitaka juhudi za haraka zifanyike kupata makubaliano yatakayosaidia kuwarejesha nyumbani ndugu zao wanaoendelea kushikiliwa mateka na kundi la Hamas.

Maandamano ya kuishinikiza serikali ya Israel ifanye haraka kupata makubaliano ya kuwarejesha mateka nyumbani 10.08.2024 Picha: Mostafa Alkharouf/Anadolu/picture alliance

Soma zaidi: Vifo vyapindukia 40,000 Gaza

Tukisalia katika mzozo huo, jeshi la Israel Ijumaa limewataka wakaazi wa kaskazini mwa mji wa Khan Younis na mashariki mwa Deir al- Balah katika Ukanda wa Gaza waondoke mara moja kabla ya kuanza kwa operesheni zake mpya. Amri hiyo ya Israel imetolewa baada ya mashambulizi ya roketi yanayodaiwa kufanywa kutoka maeneo hayo kuielekea Israel

Vita katika Ukanda wa Gaza vilichochewa na shambulio la Hamas la Oktoba 7 ambapo wanamgambo hao waliuvamia upande wa Kusini mwa Israel na kuwauwa zaidi ya watu 1,000. Wengine 250 walichukuliwa mateka kwa mujibu wa mamlaka za Israel.