Mbabazi: Waziri mkuu wa Museveni aliyegeuka hasimu
25 Januari 2016Jina lake kamili ni John Patrick Amama Mbabazi, lakini hujuilikana zaidi kama Amama Mbabazi. Alizaliwa Januari 16, mwaka 1949 kwenye kijiji cha Mparo katika kaunti ya Rukiga, iliyoko katika wilaya ya sasa ya Kabale.
Mbabazi alisoma katika taasisi mbili maarufu nchini Uganda wakati wa kipindi cha ukoloni na baada ya ukoloni- Chuo cha Kigezi kilichoko Butobere ambako alisomea masomo yake ya sekondari, na kisha shule ya Ntare alikosemea masomo ya juu ya sekondari. Mbabazi ana Shahada ya Kwanza ya Sheria aliyoipata kwenye Chuo Kikuu cha Makerere.
Mwaka 1976 alipata diploma ya uzamili ya Sheria kutoka kituo Chuo cha Maendeleo ya Sheria mjini Kampala. Mbabazi ni wakili wa Mahakama za Uganda na tangu mwaka 1977 amekuwa mwanachama wa chama cha wanasheria wa Uganda.
Taaluma, kazi na siasa
Kabla ya kujiunga na siasa, alifanya kazi kama wakili wa taifa katika ofisi ya Mwansheria Mkuu kuanzia mwaka 1976 hadi 1978, na kisha kupanda cheo na kuwa katibu wa Baraza la Sheria la Uganda kuanzia mwaka 1977 hadi 1979.
Kati ya mwaka 1986 na 1992, alifanya kazi kama mkuu wa Shirika la Usalama wa ndani. Pia alikuwa Waziri wa nchi katika Ofisi ya Rais, anayeshughulikia masuala ya siasa. Kati ya mwaka 1986 na 1992, alikuwa naibu waziri wa Ulinzi. Baada ya hapo aliteuliwa kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda kuanzia mwaka 1998 hadi 2001. Mwaka 2004, aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali na Waziri wa Sheria.
Mbabazi alishikilia wadhifa huo hadi alipoteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi mwaka 2006, nafasi aliyoishikilia hadi alipoteuliwa kuwa Waziri wa Usalama, kuanzia Februari mwaka 2009 hadi Mei 2011, wakati alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Uganda.
Alikuwa katibu wa kundi la wawakilishi wa NRM katika Bunge la Katiba ambalo liliandaa Katiba ya Uganda mwaka 1995, na alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama cha National Resistance Movement (NRM) kuanzia Novemba mwaka 2005 hadi Januari, 2015.
Waziri Mkuu chini ya Museveni
Mbabazi ni waziri mkuu wa 10 katika historia ya Uganda na alitoa mchango muhimu katika harakati za ukombozi za Uganda kutoka tawala za kidhalimu kuanzia mwaka 1972 hadi 1986 na ni mwanachama mwanzilishi wa chama tawala cha NRM.
Mbabazi amekuwa mbunge wa jimbo la Kinkiizi Magharibi katika wilaya ya Kanungu, nafasi aliyoishikilia tangu mwaka 1996.
Rafiki wa utotoni wa Mbabazi, Ruhakana Rugunda aliteuliwa na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, kushika nafasi ya Mbabazi kama Waziri Mkuu, Septemba 18, mwaka 2014. Hatua hiyo ilionekana na wengi kama njia ya Rais Museveni kumuadhibu Mbabazi baada ya kuwepo uvumi kuwa anataka kugombea urais.
Juni 15 mwaka 2015 Mbabazi alitangaza nia yake ya kuwania nafasi ya kuteuliwa kugombea urais dhidi ya Rais Museveni ndani ya chama cha NRM, wakati wa mkutano wa chama hicho Oktoba 4 mwaka 2015.
Julai 31, baada ya kuwepo kutoelewana na kutokubaliana kwa kiasi kikubwa kati ya maafisa waandamizi wa chama hicho na Mbabazi mwenyewe, waziri huyo mkuu wa zamani wa Uganda alitangaza kuwa atasimama kama mgombea binafsi. Tangazo hilo lilijibiwa na Rais Museveni, alielitaja kama "mwenendo mbaya ulioonyeshwa mapema na Mbabazi."
Mbabazi anaungwa mkono na muungano wa Democratic Alliance unaojumuisha vyama kadhaa vya upinzani nchini Uganda, pamoja na makundi ya wanaharakati na watu mashuhuri.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo
Mhariri: Iddi Ssessanga