Mbabe wa kivita wa Kongo atishia kuanzisha upya mapambano
16 Julai 2025
Amesema aidha kwamba mazungumzo hayo yanafungulia milango wageni kuingia nchini humo kupora rasilimali za nchi badala ya kuleta amani hasa Mashariki mwa nchi hiyo.
Katika kikao cha waandishi wa habari mjini Kampala siku ya Jumatano, Lubanga ametisha kuanzisha tena mapambano ya kijeshi dhidi ya utawala wa rais Tshisekedi ambaye licha ya kuwasiliana naye mara kadhaa kuhusu masuala nyeti ya kuleta amani ya kudumu amendelea kumpuuza.
Kila wakati jina Thomas Lubanga linahusishwa na harakati za kijeshi na kisiasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameibuka tena na kufahamisha kuwa angali mdau muhimu katika siasa za DRC chini ya vuguvugu lake la Mjumuiko wa Kimapinduzi CRP.
Amepongeza mazungumzo yanayoendelea huko Doha, kati ya serikali ya rais Tshisekedi na kundi la AFC/M23. Lakini anachokosoa ni kwamba maafikiano kati ya Marekani, DRC na Rwanda yamejikita zaidi katika namna rasilimali za Kongo za madini zinavyoweza kutumiwa bila kusababisha mgogoro miongoni mwa makundi mbalimbali.
Lubanga alikuwa mshtakiwa wa kwanza wa ICC, 2012
Ikumbukwe kuwa Thomas Lubanga ndiye alikuwa mtu wa kwanza kushitakiwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya ICC mwaka 2012 kwa uhalifu dhidi ya ubinaadamu na uhalifu wa kivita. Kwa zaidi ya miaka 20 amekuwa akihusishwa na harakati "za kuikomboa DRC" na kuleta amani nchini humo. Lakini kwa baadhi ya raia wa Kongo, yeye alikuwa miongoni mwa wale waliochochea vita.
Lubanga analalamika kuwa kundi lake limetengwa katika mchakato wa kuleta amani DRC na hadhani kama kuunaweza kuwa na suluhu kwenye suala la utawala wa nchi hiyo, ikiwa wadau muhimu kama yeye hawatahusishwa.
Baada ya kutumikia kifungo cha ICC cha miaka 14 alichohukumiwa 2020, Lubanga alitafuta hifadhi ya kisiasa Uganda. Uganda imekosolewa mara kadhaa kuwa inamsaidia katika harakati zake. Lakini Lubanga anakana madai hayo akisema hakuna sheria zozote za kimataifa zilizokiukwa katika kumpa hifadhi.
Hadi wakati wa kuandaa taarifa hii, serikali ya Uganda kupitia kwa jeshi na wizara ya masuala ya kigeni walikuwa hawajatoa tamko kuhusu hatua ya Lubanga kuelezea kuwa ana nia ya kuendesha mapambano dhidi ya utawala wa DRC.