Mbilikimo wabaguliwa jamhuri ya kidemokrasi ya Congo
22 Agosti 2006Uchaguzi uliyofanyika katika jamhuri ya kidemokrasi ya Congo hapo Julai 30, ang’ alau uliwatambua watu wa kabila dogo la Mbilikimo mashariki mwa nchi kuwa raia wa Congo kikamilifu. Bibi Salome Ndavuma anasema alikuwa na furaha kubwa mpaka kacheza baada ya kupiga kura. Kwani hakuamini kuwa siku kama hiyo kweli ingefika.
Japokuwa Mbilikimo hao pamoja na kabila jingine la Batwa ni wenyeji wa misitu mikubwa ya Ikweta katika eneo zima la Afrika ya kati, wamepuuzwa kijamii na kubaguliwa na makabila mengine. Kabwana Mwendanabo ambae ni jirani yake bibi Ndavuma, anasema na hapa ninamnukuu:
´´ Watu wanatuona sisi kama magorilas na wala siyo binaadamu´´ Mwisho wa kumnukuu.
Hali hiyo iliwaweka katika hali mbaya ya kulengwa kwa urahisi kwa mauwaji, ubakaji na hata kuliwa nyama wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyolisibu eneo la mashariki ya Congo. Katika misitu ya eneo hilo, Mbilikimo hao wanakaa pamoja na sokwe wanaolindwa na sheria za kimazingira. Kwa bahati mbaya sehemu hiyo ni makaazi pia ya wamamgambo kutoka Rwanda Interahamwe ambao wanashutumiwa kuhusika na janga la mauwaji ya kuangamiza jamii ya Watutsi mwaka wa 1994.
Bibi Chiza Mwemdena anasema: ´´Siku mmoja nilikamatwa na wanamgambo hao na kulazimishwa kutembea kwa miguu usiku kucha. Hatimae nilibakwa na wanamgambo wasiyopungua 30 na kuambukizwa virusi vya ukimwi. Tokea hapo sijalala tena na mume wangu´´.
Kwa sasa, hali ya usalama imeboreka kiasi katika mashariki ya Congo ingawa wanamgambo hao bado wako hapo.
Bibi Ndavuma anasema kuwa zamani walikuwa wakilala porini kuepuka mashambulizi lakini kwa sasa wanaweza kulala majumbani kwao. Hayo anasema ni matunda ya siasa ya rais Joseph Kabila na ndiyo sababu Mbilikimo walimchagua Kabila wakimtaka hata hivyo kuwafurusha kutoka Congo wanamgambo hao wa Rwanda Interahamwe.
Wafannyakazi wa mashirika ya misaada wanasema kuwa hadi sasa watu zaidi ya 1,000 wanakufa kila siku katika jamhuri ya kidemokrasi ya Congo kutokana na njaa na maradhi.
Gazeti linalochapisha maswala ya kiganga nchini Uingereza la Lancet linasema kuwa Mbilikimo ndiwo wanakufa kwa wingi ukilinganisha na watu kutoka makabila mengine kutokana hasa na malaria na maradhi ya kuhara damu. Idadi ya watoto wanaofariki dunia wakiwa na umri mdogo ni mara mmoja na nusu kubwa kuliko katika kabila la majirani zao wa Kibantu.
Nchini Uganda idadi ya watoto wanaofariki dunia ilipungua kutoka kwa asili mia 59 hadi 18 baada ya Mbilikimo kupata ardhi ya kulima.
Matumaini kwa Mbilikimo hao wa Congo ni kwamba sheria itageuka kuwapa ardhi na haki zaidi kama wananchi wengine.