1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbinu zinazotumiwa kutokomeza Malaria Uganda

22 Aprili 2024

Wakati ulimwengu ukiadhimisha siku ya kupambana na ugonjwa wa Malaria wiki hii, juhudi za mataifa yanayokumbwa zaidi na vifo na miripuko ya ugonjwa huo kama vile Uganda, zimefaulu angalau kwa kiwango fulani.

Mbu-malaria
Mbu anayeaneza MalariaPicha: PongMoji/IMAGO

Uganda ambayo iko katika nafasi ya tatu barani Afrika kwa kuwa na idadi ya wagonjwa na vifo imewekeza katika mbinu kadhaa kupambana na ugonjwa huo.

Ila baadhi ya jamii bado wanakwamisha juhudi hizo kwa kutumia vibaya vifaa wanavyopewa. Kwa mfano baadhi ya watu hutumia vyandarua vya mbu kuvulia samaki au kuvigeuza kuwa uzio dhidi ya ndege wanaoharibu mashamba yao.

Chanjo ya Malaria: Chanjo ya malaria inafanya vizuri Afrika

Afrika hujumuisha asilimia 95 ya wagonjwa wa malaria duniani. Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani, WHO mataifa 10 barani Afrika na nchi ya India ndiyo yalio na idadi kubwa ya vifo na visa vya wagonjwa wa homa ya malaria.

Uganda inashikilia nafasi ya tatu barani Afrika ikiifuata Nigeria. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ndiyo inaongoza. Waziri wa Afya dokta Jane Ruth Aceng anathibitisha hali hiyo huku akielezea kuwa vita dhidi ya malaria vinatakiwa kumuhusisha kila mtu katika jamii.

Mbu aina ya Anapheles anayeambukiza MalariaPicha: picture-alliance/dpa

''Hii ina maana kuwa tatizo la malaria Uganda ni la kiwango cha juu, kwa hiyo hata idadi ya vifo ni ya juu. Ndiyo sababu sisi kama Uganda tunatakiwa kushirikiana kama jamii kupambana na tatizo hili la malaria.''

Ijapokuwa idadi ya wagonjwa wa malaria nchini Uganda imeshuka kutoka asilimia 42 ya idadi ya watu mwaka 2009 hadi chini ya aslimia 9 kwa sasa, takwimu za wizara zinaonyesha kuwa  watu 16 hufariki kila siku nchini humo kutokana na ugonjwa huo unaoambukizwa na mbu.

Soma: Cape Verde yatangazwa kutokomeza ugonjwa wa Malaria

Wizara ya afya ikishirikiana na mashirika mbalimbali ya kimataifa imeendesha shughuli kadhaa za kukabiliana na ugonjwa huo na angalau juhudi hizi zimezaa matunda, kama anavyofafanua zaidi Dokta Jimmy Opigo, kamishna msaidizi anayesimamia shughuli za kukabiliana na homa ya malaria kama alivyozungumza na DW.

''Nchini Uganda kila familia ina chandarua cha mbu, familia pia hujigharamia kupambana na malaria kwa kununua dawa za kupuliza au kujipaka. Tuna viwanda vya vyandarua, vya dawa za malaria na pia vile vinavyotengeneza vifaa vya kupima malaria.''

Hata hivyo, baadhi ya watu hasa kwenye maeneo ya maziwa na mito hutumia vyandarua vya mbu kama nyavu za kuvulia samaki au kuvigeuza uzio dhidi ya ndege wanaoharibu mashamba yao. Dokta Daniel Kyabayinze ni mkurugenzi wa afya ya umma katika wizara hiyo.

''Tunapaswa kuwaambia watu watumie vyandarua kwa njia iliyokusudiwa. Malaria inaweza kuwaua na pesa wanazochuma kwa kutumia vibaya vyandarua hazitayaokoa maisha yao.''

Siku ya Malaria duniani

02:20

This browser does not support the video element.

Shirika la WHO linaeleza kuwa duniani, kila dakika moja mtoto mmoja mwenye umri wa chini ya miaka mitano hufariki kutokana na homa ya malaria. Idadi kubwa ya vifo hivyo ni barani Afrika. Katika wiki chache zijazo Uganda itatoa chanjo dhidi ya malaria kwa watoto ikijiunga na mataifa mengine ya Afrika yaliyotangulia kama vile Kenya mwaka 2019. Lakini waziri wa afya Jane Ruth Aceng anatahadharisha kuwa chanjo hiyo haitoi kinga kwa watoto wote wanaoipata.

''Kwa watoto, chanjo hiyo ina kinga ya asilimia 50 tu. Kwa hiyo siyo suluhisho lenye uhakika, suluhisho la uhakika tunalotegemea ni kuzidisha juhudi za kijamii.''

Uganda pia inazingatia kurejelea mpango wa kunyunyiza viwatilifu vya kuangamiza mbu hata kama itakuwa DDT ambayo mataifa ya Ulaya yalitumia kuangamiza malaria.Kamerun yazindua kampeni ya kihistoria ya chanjo ya Malaria Jitihadi za awali za kutumia mbinu hiyo zilipingwa na wanasiasa. Waziri Aceng anadai kuwa wanasiasa hao walichochewa na makampuni yanayouza dawa za kutibu malaria yakihofia kuwa yangepoteza soko la dawa zao. 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW