Mbio za kuwania nafasi ya waziri mkuu Japan zaanza
30 Agosti 2020Mbio hizo zimepamba moto kuwania kiti cha waziri mkuu Abe ambaye ametumikia wadhifa huo akiwa kiongozi wa Japan ambaye ametumikia kwa muda mrefu zaidi.
Suga, mfuasi wa muda mrefu wa Abe katika jukumu muhimu la msaidizi , aliwahi kukana kuwa na nia ya kiti hicho lakini alivutia shauku kutokana na mahojiano kadhaa , na shirika la habari la Reuters na mashirika mengine ya habari, katika siku kadhaa kabla ya Abe ghafla kutangaza kujiuzulu kutokana na sababu za kiafya.
Serikali ya Suga itaendeleza mipango ya bajeti na kuchochea uchumi ambayo yalikuwa ni dira ya utawala wa Abe wa karibu miaka minane madarakani.
Tangazo la Abe siku ya Ijumaa , akielezea kuhusu kudhoofika kwa hali yake ya kiafya, iliweka uwanja wazi kwa uchaguzi wa kiongozi ndani ya chama cha Liberal Democratic. Rais wa chama cha LDP ana hakika ya kuwa waziri mkuu kwasababu ya wingi wa wabunge wa chama hicho katika bunge.
Suga aliamua kujiunga na mbio za kuwania kuwa kiongozi wa LDP akisema anapaswa kuchukua jukumu la mbele kutokana na matarajio ya uwezo wake wa kushughulikia matatizo, kama janga la COVID-19 pamoja na kuporomoka kwa kiasi kikubwa uchumi wa Japan tangu vita vikuu vya dunia, shirika la habari la Kyodo limesema, likinukuu chanzo ambacho hakikutajwa.
Simu zilizopigwa katika ofisi ya bunge ya Suga zikitaka tamko kutoka kwake hazikupokelewa.
Suga atajiunga na wagombea wengine kama waziri wa zamani wa mambo ya kigeni Fumio Kishida na waziri wa zamani wa ulinzi Shigeru Ishiba.
Waziri wa mazingira Shinjiro Koizumi, mwenye umri wa miaka 39, mtoto wa waziri mkuu wa zamani Junichiro Koizumi na anayefikiriwa kuwa waziri mkuu wa baadae, ameamua kutoshiriki katika mbio hizi, lakini atamuunga mkono waziri wa ulinzi Taro Kono, iwapo atajiunga na mbio hizo, kituo cha taifa cha redio na televisheni , NHK kimesema.
Waziri wa zamani wa mambo ya ndani Seiko Noda na waziri wa zamani wa ulinzi Tomomi Inada, ambaye anafahamika kuwa mpenzi mno wa masuala ya bajeti, wanania ya kutaka kuwa wanawake wa kwanza nchini Japan kuwa mawaziri wakuu, vyombo vya habari vimeripoti.