Mbio za mwenge wa Olimpiki kuanzishwa bila mashabiki
15 Machi 2021Watazamaji watazuiwa kushudia tukio la kuanzishwa mbio za mwenge wa Michezo ya Olimpiki ya Tokyo mnamo Machi 25. Waandalizi wa tamasha hilo maarufu la michezo ulimwenguni wametangaza hayo leo wakati siku zikianza kuhesabiwa tayari kwa Michezo hiyo iliyoahirishwa mwaka jana kutokana na janga la corona.
Hafla hiyo ya mbio za mwenge wa Olimpiki haitahudhuriwa na umma, lakini matukio hayo yataonyeshwa moja kwa moja kwenye intaneti. Takriban mashabiki 3,000 walitarajiwa kushiriki mbio za mwenge huo zitakazomalizika Julai 23 katika sherehe ya ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki
Uamuzi wa kama mashabiki wa kigeni wataruhusiwa kuingia Japan kwa ajili ya Michezo hiyo unatarajiwa kufanywa kabla ya Machi 25. Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki – IOC Thomas Bach alizungumzia suala hilo "Jnga hili litahitaji kila mmoja wetu ajitolee. familia za wanamichezo tayari zililazimika kufanya maamuzi magumu ya aina hiyo kwenye matukio yote ya karibuni, kwa sababu mengi yalifanyika bila mashabiki, na pia bila familia zao na marafiki. Hili ni moja ya mambo ambayo ninawahurumia wanamichezo, familia zao, marafiki zao lakini tunapaswa kuweka usalama mbele.
AFP, DPA, AP, Reuters