1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbowe: Chadema itaendelea kuikosoa serikali Tanzania

Veronica Natalis
6 Machi 2023

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chama cha Demokrasia na Maendelea - Chadema, kimesema kitaendelea kuikosoa serikali iliyopo madarakani pamoja na kuendeleza mchakato wa kudai katiba mpya.

Chadema Chairman Freeman Mbowe
Picha: Ericky Boniphace/DW

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe alitoa kauli hiyo wakati tayari kukiwa na mchakato wa maridhiano baina ya chama chake na serikali, mchakato kuo ukiacha maswali kwa baadhi ya watu kama ni maridhiano kwa ajili ya vyama vya siasa au kwa ajili ya wananchi.

Mbowe amesema maridhiano hayo hayazuii chama chake kuikosoa serikali na kuendeleza mapambano ya kukijenga chama chake kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025.

Bado kuna matatizo mengi, na hsimanishi kwamba kukiwa kunamaridhiano kwakua tunazungumza na mama, waziri mkuu au serikali ndio tutasitisha wajibu wetu wa kuikosoa serikali hapana," alisema Mbowe, na kuongeza, "wajubu wetu upo pale pale, hatutaogopa kuikosoa serikali na hatutaogopa kueleza sera zetu mbadala kama chama cha upinzani."

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe akiwa katika mazungumzo na mwandishi wa DW Dotto Bulendu, Januari 22, 2023 mjini Mwanza, Tanzania.Picha: Dotto Bulendu/DW

Soma pia: Je ni sahihi Chadema kujiondoa katika uchaguzi Tanzania?

"Na dhamira yetu ya kuing'oa CCM madarakani ipo pale pale, maridhiano hayaondoi dhamira hiyo. Hatupo hapa kuisindikiza CCM eti ifanye vizuri zaidi kama anavyosema mama, wao wanaweza kufanya vizuri lakini sisi tunauwezo wa kufanya vizuri zaidi ya wao kwa sababu wao wameshindwa kufanya vizuri kwa zaidi ya miaka 60 tangu CCM ianze kuliongoza taifa letu."

Samia kuhudhuria sherehe za Chadema

Wakati hayo yakijiri, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, naye alikuwa jijini Arusha ambapo wakati akizungumza na hadhara maeneo ya USA River katika jiji hilo la kitalii, alinukuliwa akisema wapinzani sio maadui, bali wanamsaidia kuijenga CCM.

"Tunachotofautiana ni mawazo tu na fikra, lakini pia mimi sichukulii wapinzani kama maadui, nawachukulia kama watu watakaonuonesha ni wapo changamoto zilipo ili nizitekeleze ili CCM iimarike," alisema Rais Samia.

Rais Samia Suluhu Hassan amesema wapinzani siyo maadui wa CCM bali wanamsaidia kukiimarisha chama.Picha: Ericky Boniphace/DW

Soma pia: Mwanasiasa wa upinzani Lema arejea Tanzania kutoka uhamishoni

"Kwa hiyo Mdogo wangu Lema aliniambia mama nataka kurudi, kasema mama nina kesi nikamwambia nazifuta rudi. Amerudi tuimarishe siasa, mwanamke ni yule anayejiamini. Kwenye siasa tunajiamini na mwendo ni huo huo mpaka 2025, tunawathamini na tunawatambua."

Rais Samia anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za maadhimisho ya siku ya wanawake duniani tarehe nane Machi mwaka huu, ambazo zimeandaliwa na Chadema, tukio ambalo linaendelea kuweka alama ya ushirikiano miongoni mwa vyama hivyo vya siasa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW