1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbowe kuachia uenyekiti wa Chadema kwa Lissu?

18 Desemba 2024

Mwenyekiti wa chama Kikuu cha upinzani Tanzania, Chadema, Freeman Mbowe, ametoa saa 48, akieleza kuwa baada ya saa hizo, ndipo atatoa jibu la iwapo atatetea kiti chake cha uenyekiti wa taifa wa chama hicho au la.

Viongozi wa upinzani Tanzania mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe (kulia) akiwa na Tundu Lissu (kushoto)
Viongozi wa upinzani Tanzania mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe (kulia) akiwa na Tundu Lissu (kushoto)Picha: Eric Boniface/DW

Mbowe ameyasema hayo Jumatano mara baada ya kundi la wafuasi wa chama hicho wakiwamo wenyeviti wa mikoa  kukusanyika nyumbani kwake na kumsihi  kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo.

Atagombea au hatagombea, hilo ndilo swali linalotikisa mioyo ya watanzania na wafuasi wa CHADEMA, mara baada ya Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Freeman Mbowe, kutoa saa 48 za kutafakari kabla ya kufanya maamuzi na kutoa majibu.

“Jumamosi nitazungumza neno langu la mwisho na wahariri wa habari, saa 5 asbh, nitazungumza na wahariri hapa hapa ktk ukumbi huu, kutoa kauli ya mwisho mwenyekiti mbowe naamua nini,” alisema Mbowe.

Wenyeviti wa mikoa wakusanyika nyumbani kwa Mbowe

Kadhalika Mbowe akitoa hotuba yake mbele ya mamia ya wafuasiwa CHADEMA, alitumia wasaa huo kuwaomba wana CHADEMA kutotumia lugha ya matusi katika kampeni za uchaguzi wa ndani wa chama na kusema hata yeye anatangaza msamaha kwa wote wanaotoa taarifa za upotoshaji dhidi yake na dhidi ya chama. 

Freeman Mbowe akizungumza katika mkutano Dar es SalaamPicha: Eric Boniface/DW

"Kama Mwenyekiti mwandamizi wa chama hiki, nitaangalia mwenendo wa kampeni kati ya leo mpaka   jumamosi na kesho, nikiona chama change kinaelekea kuzamishwa, kamanda naingia mzigoni,” alisema Mbowe.

Awali, kabla ya Mbowe kutoa tamko, kundi la wanachama wa CHADEMA wakiwamo wenyeviti wa mikoa na Baraza la Wanawake wa chama hicho, (BAWACHA) walikusanyika nyumbani kwa Mwenyekiti huyo na kueleza kuwa nia yao ya kufika katika makazi ya Mbowe ni kumshawishi kuchukua fomu na kuwania uenyekiti wa CHADEMA.

Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Iringa, William Ngai,alizungumza kwa niaba ya wenyeviti wa mikoa wa CHADEMA na kusema,

"Tunazidi kukua kwenye hiki chama , tunazidi kukua kwenye mamlaka lakini  mtu anayeweza kututawala kwa sasa ni jenerali mkuu, Freeman Aikael Mbowe," alisema Ngai.

Mapema kuanzia saa  tano asubuhi, ilionekana misafara ya pikipiki, baiskeli na waenda kwa miguu ikienda nyumbani kwa Mbowe, wote hao wakiwa wamevalia sare za CHADEMA na baadhi wakishikilia bendera.

Upinzani dhidi ya Mbowe

Desemba 12, Makamu Mwenyekiti  wa CHADEMA Bara, Tundu Lissu alitangaza rasmi nia yake ya kuwania nafasi ya Uenyekiti ngazi ya Taifa ndani ya CHADEMA.

Tundu Lissu akizungumza na waandishi wa habariPicha: Emmanuel Herman/REUTERS

Jana Lissu alichukua rasmi fomu ya kuwania nafasi hiyo ya uongozi na kukabidhiwa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika na leo ameirudisha na ikapokelewa Naibu Katibu Mkuu Bara, Benson Kigaila.

Kumekuwa na upinzani mkubwa dhidi ya Mbowe kuendelea kukiongoza chama hicho kwa kile kinachoelezwa ameshikilia Madaraka kwa miaka zaidi ya 20.

Viongozi waliowahi kukiongoza CHADEMA katika miaka 33  ya uhai wa chama hicho, ni Edwin Mtei, mwanzilishi wa chama hicho, na baadaye Bob Makani na Mbowe, anayeshikilia nafasi hiyo kuanzia 2004 mpaka sasa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW