1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbowe: Mifarakano ya CHADEMA ni jambo la kawaida

19 Novemba 2024

Mwenyekiti wa chama kikuu cha Upinzania Tanzania, CHADEMA, Freeman Mbowe amesema mifarakano ndani ya chama hicho ni jambo la kawaida na kuwa chama cha siasa kisichokuwa na kile alichookita minyukano ni chama mfu.

Internationaler Tag der Demokratie, Tansania
Freeman Mbowe Mwenye mwenyekiti wa Taifa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), na Mwenyekiti wa sasa wa TCD.Picha: Florence Majani/DW

Ameyasema hayo ikiwa ni siku chache baada ya kuwepo kwa kauli tata kutoka kwa viongozi wengine wa chama hicho. Mbowe ameyatoa matamshi hayo leo mchana katika mkutano na wanahabari na kueleza kuwa kuna wakati viongozi ndani ya chama wanatofautiana kauli na wanakwenda mbali zaidi, lakini kama chama wanayamaliza ndani kwa ndani.

Mbowe ameyasema hayo ikiwa ni siku chache baada ya Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania, Bara Tundu Lissu, kunukuliwa na vyombo vya habari akikishushia chama tuhuma za rushwa, mikanganyo ya uchaguzi wa serikali za mitaa na akiweka wazi kukerwa kwake na kile alichosema maridhiano ya uongo kati ya serikali na CHADEMA.

Tundu Lissu kuanza kampeni ya serikali za mitaa Jumatano

Kadhalika Mbowe amesema wakati hayo yakijiri Tundu Lissu anatarajiwa kuanza kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa kesho wilaya ya Ikungi na baadaye Tarime.

Wiki iliyopita CHADEMA kilitoa taarifa kwa umma kikijibu hoja za Lissu, bila ya kumtaja moja kwa moja na kusema chama hicyho hakijawahi kuletewa hoja ya kugawana majimbo au nafasi za madaraka kutoka kwa serikali.

Awali, Mbowe alielezea hali jumla ya mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa ambao unafanyika Novemba 27 akisema wagombea wa CHADEMA waliopitishwa kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa serikali za mitaa ni asilimia 33.2 sawa na theluthi moja ya wagombea wote huku akiendeleza msimamo wa chama hicho wa kutojiengua.

Awali, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John John Mnyika alitumia fursa hiyo mbele ya wanahabari kukanusha kauli iliyotolewa juzi na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, TAMISEMI Mohamed Mchengerwa ya kuwa vyama vyote 19 vya siasa nchini vilikubaliana katika hatua zote za uchaguzi.

Soma zaidi:Afisa wa juu wa CHADEMA atekwa na kujeruhiwa Tanzania

Uchaguzi wa serikali za mitaa katika taifa hili la Afrika Mashariki unafanyika mnamo Novemba 27, katika mazingira ambayo hayapishani sana na ule wa mwisho wa mwaka 2019, ambapo chama kinachotawala CCM kilijizolea takribani viti vyote, kutokana na wagombea wa upinzani kushindwa kuwania kwa sababu zinazofanana na hizo.