Walinzi wawili wa mbunge wa Somalia wauwawa mjini Mogadishu
5 Aprili 2016Kulingana na Mkuu wa polisi mjini Mogadishu Ibrahim Mohammed, mbunge huyo Mohamed Ali Deheye alijeruhiwa na watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki katika eneo la Hamarweyne. Mkuu huyo wa polisi amesema uchunguzi kwa sasa unafanyika lakini pia bado kuna watu wengine waliojeruhiwa katika mkasa huo.
Waliofanya kisa hicho wanasemekana kulizuwia gari la mbunge Ali Deheye kisha kuanza kulimiminia risasi, walinzi wake wawili walifariki papo hapo.
Aidha wanamgambo wa Al Shabaab kupitia taarifa iliyotangazwa na kituo chake cha redio cha Andalus, wamekiri kufanya jaribio la kumuua mbunge huyo.
Wanamgambo hao walioondolewa kwa nguvu katika mji mkuu wa Mogadishu mwaka wa 2011 bado wanaendelea kudhibiti maeneo mengine huku wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara ya mabomu na ufyatuaji risasi mjini Mogadishu na sehemu nyengine Somalia.
Wakati huo huo kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika pamoja na serikali ya Somalia wamewauwa maafisa wakuu wa kundi hilo la Al Shabaab linalofungamanishwa na kundi la kigaidi la Al Qaeda. Mauaji hayo yanasemakana kufanyika siku chache zilizopita.
Licha ya kundi hilo la kigaidi kushambuliwa bado linadhibiti maeneo ya mashambani na wanaendelea na mashambulizi yao yanayolenga kuisambaratisha serikali ya nchi hiyo inayoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa.
Amisom yatangaza kuwauwa viongozi kadhaa wa Al Shabaab
Kikosi cha Amisom kimesema viongozi wa Al Shabaab waliouwawa ni pamoja na kamanda wa kundi hilo na naibu wake waliyoko mjini Janaale, Abdirashir Bugdube na Sheikh Mohamed Ali. Kamanda mwengine wa kundi hilo katika eneo la Leego, Aden Bale pia aliuwawa.
Mwengine ni jaji wa Al Shabaab katika mji huo wa Janaale, Mohamed Abribao, raia mmoja wa Yemen anayelitengenezea mabomu kundi hilo anayejulikana kama "Abu Islam" na mwanamume mmoja aliyetambuliwa kama mtoa mafunzo mkuu wa kundi hilo Sheikh Mansur, hii ikiwa ni kwa mujibu kwa taarifa iliyotolewa na Amisom siku ya Jumanne.
Pia inasemekana Amisom ikisaidiana na kikosi cha serikali ya Somalia walimuua Hassan Ali Dhoore, mkuu wa ujasusi wa kundi la al Shabaab katika eneo la Shabelle. hata hivyo ikulu ya Marekani awali ilisema ilimuua kiongozi huyo Hassan Ali Dhoore katika shambulizi lake la angani lililofanyika tarehe 31 mwezi Machi mwaka huu.
Huku hayo yakiarifiwa msemaji wa jeshi la Al Shabaab Abdiasis Abu Musab, amesema ni Dhoore pekee aliyeuwawa huku akipuuzilia mbali ripoti nyengine za vifo vya viongozi wa al Qaeda akizielezea ripoti hizo kama propaganda.
Aidha AMISOM kwa sasa imesema ipo katika harakati ya kuondoa mabomu yote katika eneo la Janaale.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/REUTERS
Mhariri: Daniel Gakuba