1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbunge mwengine wa upinzani Tanzania ahamia chama tawala

George Njogopa31 Julai 2018

Kwa mara nyingine, mbunge mwengine wa upinzani amekihama chama chake cha upinzani na kujiunga na chama tawala CCM.

Tansania Parlament Dodoma - Parlamentsvorsitzende mit Philip Mpango und Premierminister Kassim Majaliwa
Picha: DW/S. Khamis

Wimbi la wabunge wa upinzani nchini Tanzania kuhamia chama tawala CCM limeibuka tena baada ya jana usiku mbunge wa chadema katika Jimbo la Monduli, Julias Kalanga kukihama chama chake hicho na kujiunga na chama hicho tawala. Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya mbunge mwingine katika Jimbo la Ukonga jijini Dar es Salaam kukitupa mkono wa kwa heri chama chake akikimbilia CCM. 

Bila kupoteza wakati wanasiasa hao walioonekana kuwa na misimamo mikali wakati wakiwa kambi ya upinzani tayari wameanza kupanda majukwaa ya CCM katika kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani na mbunge unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo.

Kuondoka kwa wabunge hao kunazidi kupunguza idadi ya wapinzani bungeni ikiwa ni wabunge wanne kujiunga na chama hicho tawala tangu kuanza kwa vuguvugu la wanasiasa kubadilisha vyama katika kile wanachodai kuunga mkono juhudi za rais John Magufuli.

Katika hali isiyotarajiwa na wengi, mbunge wa Monduli jimbo ambalo kwa miaka mingi ilikuwa kambi ya aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Ukawa, Edward Lowassa alitangaza kukipa mkono wa kwaheri chama chake hicho na kujiunga na CCM.

Tangu kuanza kwa vuguvugu la wanasiasa kubadilisha vyama katika kile wanachodai kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli, wabunge wanne wa upinzani wamejiunga na CCM.Picha: Imago/Xinhua Afrika

Tukio hilo lililofanyika usiku wa Jumatatu limewashtua wengi hasa kutokana na uzito wa jimbo hilo. Aliyekuwa wa kwanza kukata utepe katika vuguvuvugu hili la awamu ya pili alikuwa aliyekuwa mbunge wa Ukonga,Mwita Waitara ambaye sasa yuko kwenye kampeni za ccm kunadi wagombea wake katika kampeni za udiwani na ubunge.

Waitara ambaye wakati Fulani alikuwa mkosoaji mkubwa wa CCM pamoja na watendaji wake bungeni, alisema alimejiondoa ndani ya chadema akiwatuhumu viongozi wake.

Kujiondoa kwa wabunge hao kunamaanisha kwamba majimbo waliyokuwa wakiyawakilisha sasa yako wazi hatua ambayo inaashiria kurejea tena kwenye mchakamchaka wa uchaguzi mwingine. Ingawa kumekuwa na maoni tofauti kuhusu hatua hiyo, baadhi ya wananchi wanaona mwenendo huu wa siasa unaweza kugharimu fedha nyingi kufanya uchaguzi wa marudio.

Ndani ya mwaka huu pekee kumefanyika uchaguzi katika majimbo mawili baada ya wabunge wake wa awali kijiunga na CCM na wamerejea tena bungeni baada ya kupitishwa na chama hicho katika uchaguzi wa marudio.

Mwandishi: George Njogopa

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW