1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbunge wa Labour aitisha maandamano kumuondoa Theresa May

15 Juni 2017

Mbunge John McDonnell amewataka watu milioni moja kujitokeza na kufanya maandamano barabarani ili kushinikiza kufanywa kwa uchaguzi wa pili utakaomuondoa Waziri Mkuu Theresa May madarakani.

London May nach Parlamentswahl
Picha: Getty Images/AFP/O. Andersen

Mwanasiasa mmoja mkuu wa chama cha Labour nchini Uingereza amewataka watu milioni moja kujitokeza na kufanya maandamano barabarani ili kushinikiza kufanywa kwa uchaguzi wa pili utakaomuondoa Waziri Mkuu Theresa May madarakani. Hayo yanajiri wakati ambapo chama cha Conservative cha Theresa May hakijaelewana na kile ya Ireland ya Kaskazini DUP kuhusu kuunda serikali.

Kulingana na ripoti katika gazeti la Daily Mirror, mbunge wa chama cha Labour John McDonnell ambaye angekuwa waziri wa fedha lau chama chake kingelishinda uchaguzi uliopita, amewahimiza waandamanaji kujitokeza barabarani kuunga mkono wito wa chama hicho cha kutaka kupunguzwa kwa fedha za matumizi serikalini, na pia kuongeza shinikizo la kutaka uchaguzi mwingine ufanywe. Gazeti hilo limesema baadhi ya makundi ya mirengo ya kushoto yanapanga maandamano makubwa tarehe mosi Julai kutia shinikizo dhidi ya bibi May.

Gazeti hilo limemnukuu McDonnell akisema kuwa "Tunawataka watu watakaofanya kila waliwezalo kuhakikisha uchaguzi unafanywa mapema iwezekanavyo" Akizungumza na wanaharakati, McDonnell amekitaka chama cha wafanyakazi TUC kuwarai watu kuitikia wito huo wa maandamano. Baada ya kushinda viti zaidi kuliko ilivyobashiriwa, kiongozi wa chama cha Labour Jeremy Corbyn alisema anataka kumuondoa bibi May madarakani.

Jeremy CorbynPicha: picture alliance/PA Wire/D. Lipinski

Kufuatia utata wa kisiasa uliosababishwa na kushindwa kwa chama cha Conservative kupata wingi wa viti bungeni katika uchaguzi ulioitishwa mapema, na hivyo kusababisha mkwamo bungeni, Waziri Mkuu Theresa May anafanya mazungumzo na chama kidogo cha Ireland Kaskazini-DUP ili kupata viti vyake kumi.

Makubaliano bado

Msemaji wa chama cha DUP amesema leo kuwa mazungumzo kati ya vyama hivyo viwili kuhusu kuunda serikali ya wachache yataendelea. Naibu mkuu wa chama hicho Nigel Dodds anaongoza ujumbe wa chama cha DUP kwenye mazungumzo hayo jijini London baada ya kiongozi mkuu wa chama Arlene Foster kurejea Ireland Kaskazini. Dodds anatarajiwa kukutana na May leo (15.06.2017) katika mojawapo ya misururu ya mikutano ambayo bibi May anafanya na viongozi wa Ireland Kaskazini ili kufikia makubaliano.

Hata hivyo bado hakuna maelewano licha ya kiongozi wa bunge kuthibitisha kuwa hotuba ya Malkia Elizabeth wa pili itatolewa Jumatano wiki ijayo wakati wa ufunguzi rasmi wa bunge. Ufunguzi huo umecheleweshwa kwa muda wa siku mbili ili kumpa Theresa May muda wa kumaliza mazungumzo.

Kionfozi wa chama cha DUP Arlene Foster na naibu wake Nigel DoddsPicha: Getty Images/AFP/B. Stansall

Wakati hayo yakijiri, kiongozi wa chama cha kiliberali Union Liberal Party kinachopendelea Umoja wa Ulaya bwana Tim Farron amejiuzulu kutoka kwenye wadhifa wake akisema maswali kuhusu imani yake ya Kikristo yamemfanya ahisi ni vigumu kuendelea kuhudumu. Tim ameendelea kusema "Mtu mwenye hekima zaidi yangu labda angeweza kukabiliana na hili vyema kubakia kuwa mwaminifu kwa Kristo huku akiongoza chama cha siasa katika mazingira ya sasa. Kuwa mwanasiasa na kuishi maisha ya Kikristo kulingana na mafundisho ya bibilia imekuwa jambo lisilowezekana kwangu."

Chama hicho pekee ndicho kiliahidi kuitisha kura nyingine ya maoni ya ikiwa Uingereza ijiondoe katika Umoja wa Ulaya au la, lakini kilipata viti kumi na viwili pekee katika jumla ya viti 650.

Mwandishi: John Juma/RTRE/AFPE/DPAE

Mhariri: Josephat Charo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW