1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

Mbunge wa Ujerumani aukosoa mradi wa EACOP

22 Februari 2023

Siku moja tu baada ya Tanzania kuidhinisha rasmi ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kati ya nchi hiyo na Uganda, mbunge wa Ujerumani wa chama cha Kijani ameukosoa mradi huo maarufu kama EACOP.

Uganda Unterschrift EACOP in Kampala
Picha: Presidential Press Unit/Uganda

Mbunge huyo Kathrin Henneberger amependekeza mradi huo ambao unakadiriwa kugharimu kiasi cha dola bilioni tatu na nusu za Kimarekani usimamishwe mara moja baada ya kushuhudia ujenzi huo ukianzishwa kwa upande wa Uganda.

Henneberger ambaye amekamilisha ziara yake kwenye eneo la shughuli za uchumbaji mafuta magharibi mwa Uganda siku ya Jumanne, alijionea hali ilivyo na pia kufanya mashauriano na watu wa sehemu hiyo pamoja na asasi za kiraia.

Akizungumza na DW, mbunge huyo ameuelezea mradi huo kama wenye madhara makubwa kwa mazingira na vilevile kusababisha ukiukaji wa haki za binaadamu.

Walioathirika hawajaridhika na fidia

Mbali na kudai kuwa kanda ya bonde la Ziwa Albert ina ekolojia dhaifu ikiwemo mbuga za wanyama, Henneberger amefichua kuwa watu walioathirika kutokana na mradi huo hawajaridhishwa na fidia walizolipwa au kuahidiwa kulipwa na wengine wana mashaka kama watalipwa kwani tayari mradi umekwishaanza. 

Kathrin Henneberger, Mbunge wa Ujerumani kupitia chama cha KijaniPicha: Lubega Emmanuel/DW

''Hakuna aliyesema kwamba fidia inatosha. Wengi wanahofia kuwa huenda wasipate chochote kwani mradi umeanza na pesa walizoahidiwa ni kidogo mno kufidia hasara waliyoingia,'' alifafanua Henneberger.

Mbunge huyo wa chama cha Kijani aliagizwa na bunge la Ujerumani kufuatilia madai ya wanaharakati wa mazingira na wale wa haki za binadamu kuhusu madhara ya mradi huo kimazingira na kijamii.

Hii ni chini ya mkakati wa kuhakikisha haki kuhusu tabia nchi. Ameshangaa kwa nini kampuni ya Ufaransa ya Total Energies na wabia wake wameamua kuanzisha mradi huo kabla ya kupata fedha za uhakika za kuendeleza ujenzi wake. 

''Total Energies inafaa kusitisha mradi huo. Ni wazi kabisa kwamba wamechukua hatua ya kujenga bomba hilo licha ya kuwa hawana fedha na hivyo ndivyo ilivyo kwa upande wa Tanzania,'' alibainisha Henneberger.

Eeneo la Ziwa Albert, UgandaPicha: AFIEGO

Kwenye sherehe za uzinduzi wa mradi wa uchimbaji mafuta mwezi Januari mwaka huu, balozi wa Tanzania nchini Uganda Dokta Aziz Ponary Mlima alielezea kuwa kwa upande wa nchi yake, idadi kubwa ya watakaothirika na mradi huo walikwishafidiwa. 

Tanzania imelipa asilimia 86 ya fidia 

''Serikali ya Tanzania imekuwa ikiwalipa fidia watu watakaoathirika na mradi huo na hadi sasa asilimia 86 wamelipwa. Tuna matumaini kuwa kabla ya mradi huo kuanza wale wengine asilimia 14 watakuwa wamefidiwa,'' alisema Mlima.

Kwa upande wake kampuni ya Total Energies imendelea kusisitiza kwamba imezingatia sana masuala ya mazingira na kutekeleza miradi kadhaa kuhakikisha kuwa maumbile anuwai ikiwemo wanyamapori katika mbuga za wanyama yanalindwa dhidi ya uchafuzi na uharibifu kwa jumla. Imetoa mfano kuwa katika kipindi cha saa milioni kumi za kazi, hapajatokea ajali yoyote kwa wafanyakazi wake. 

(DW)
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW