1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbunge wa Ujerumani na kashfa ya rushwa manunuzi ya barakoa

Angela Mdungu
26 Februari 2021

Mbunge wa chama cha kihafidhina  cha CSU Georg Nüßlein anakabiliwa na tuhuma za rushwa kuhusu mpango wa barakoa za kujikinga na COVID 19. Anatuhumwa kupokea Euro 660,000 katika kumshawishi msambazaji wa barakoa hizo

Deutschland Bundestag
Picha: Gregor Bauernfeind/dpa/picture alliance

Bunge la Ujerumani limepiga kura ya kumuondolea kinga dhidi ya mashtaka mbunge Georg Nüßlein,kutokana na tuhuma zinazomkabili. Mbunge huyo amekuwa mtaalamu wa masuala ya afya na mbunge tangu mwaka 2002.

Waendesha mashtaka mjini Munich walithibitisha jana Alhamisi kuwa wapelelezi walivamia nyumba 13 zinazohusishwa na mbunge huyo nchini Ujerumani pamoja na Liechtenstein katika uchunguzi wao juu ya tuhuma hizo.

Mmoja wa wabunge  ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya kinga ya bunge Marco Buschmann aliandika kupitia ukurasa wake wa twitter akisema, sasa mahakama  inapaswa kufanya kazi yake.

Tuhuma dhidi ya  Georg Nüßlein ziliibuka mwaka uliopita kwa madai kuwa aliishawishi serikali kutoa tenda kwa msambazaji wa barakoa. Vyombo vya habari viliripoti kuwa kwa kufanya hivyo, alipokea Euro 660,00 sawa na dola $800,000 za kimarekani

Fedha alizopokea zilihamishiwa kwenye kampuni anayosimamia

Ripoti zaidi zinasema, fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti ya kampuni inayosimamiwa na Nüßlein, ambayo  kulingana na kituo cha habari cha RTL haikutangaza ushuru wa mapato yake.

Mapema Jumatatu, mbunge wa wa chama cha SPD  Kattja Mast aliandika pia kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa, ikiwa kuna hata fununu kwamba mbunge wa Ujerumani amenjinufaisha kutokana na janga la virusi vya corona, basi hizo ni tuhuma nzito zinazopaswa kutolewa maelezo ya kina.

Wabunge wataka uwazi kupambana na rushwa

Wabunge walimkosoa Nüßlein, mwanachama wa chama cha CSU ambacho ni chama dada wa chama cha CDU cha Kansela Merkel. Nüßlein amekuwa mbunge tangu mwaka 2002 na amefanya kazi kama naibu wa mwenyekiti wa vyama vya kihafidhina tangu mwaka 2014.

Georg Nüßlein, Mbunge wa CSUPicha: Christoph Hardt/Geisler-Fotopres/picture alliance

Chama cha SPD kinachofuata siasa za nadharia ya mrengo wa wastani wa kushoto kimetaka hatua kali zenye uwazi zichukuliwe na kuzuia rushwa kwa wabunge.

Chama hicho kilitaka wabunge waweke wazi miradi yao ya uwekezaji, mapato ya kila mwaka na SPD ilidai utangazaji wa lazima wa uwekezaji wa wabunge, mapato ya kila mwaka na kuandikisha ushawishi kwa bunge na serikali ya shirikisho.

Mwaka jana, mbunge mwingine kutoka chama cha Merkel alilalamikiwa kufanya ushawishi ulioihusisha kampuni moja ya Marekani, jambo lililoibua utata katika bunge. Kiongozi wa chama cha die Linke katika bunge, Jan Korte, alitoa wito wa kupiga marufuku wabunge kuwa washawishi wanaolipwa.