1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchakato wa amani unaoyumba Sudan Kusini wawasikitisha raia

22 Februari 2022

Imetimia miaka miwili sasa tangu rais Kiir na makamu wake Machar walipounda serikali ya umoja wa kitaifa, lakini mafanikio ya mkataba huo yangali mashakani.

Südsudan Verhandlungen zwischen Regierung und Opposition
Picha: Reuters/J. Solomun

Wakati família ya Tunda Henry na ilipoikimbia Sudan Kusini kufuatia machafuko ya wenyewe kwa wenyewe miaka mitano iliyopita, waliahidi kurudi nyumbani pindi hali itakapotulia.

Lakini kadri mkataba wa amani wa taifa hilo changa unavyozidi kuyumba, ndivyo família yake inavyozidi kupoteza matumaini ya kurudi.

Amnesty: Vita vya Sudan vinaweza kuwa uhalifu wa kivita

Tayari imeshatimia miaka miwili tangu rais Salva Kiir na makamu wake Riek Machar walipounda serikali ya umoja wa kitaifa, kulingana na makubaliano ya amani waliyosaini mwaka 2018 hivyo kusitisha machafuko yaliyosababisha vifo vya takriban watu 400,000.

Vipengee muhimu vya makubaliano ya amani havijatekelezwaPicha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Mizozo na majanga yaendelea kuizonga Sudan Kusini

Tangu wakati huo, taifa hilo changa zaidi limeendelea kuzongwa na mizozo, mafuriko, njaa, machafuko ya kikabila na misukosuko ya kisiasa, huku ahadi zao katika makubaliano ya amani zikikosa kutekelezwa. Hali ambayo imewaacha raia kama Henry wakipoteza matumaini.

Mchakato wa amani Sudan Kusini hatarini: UN

"Sina furaha,” amesema Henry, baba wa watoto watano na mtu pekee katika família yake anayeishi Sudan Kusini.

Maisha yake yanazidi kugubikwa wasiwasi na mashaka hivi kwamba anashindwa hata kufunga safari kutoka mji mkuu Juba kuenda kwao kijijini.

"Watu wengine hutoweka wakiwa njiani,” amesema Henry. Makundi ya waasi mfano National Salvation Front (NAS) ambalo halikuwa miongoni mwa makundi yaliyosaini mkataba huo bado yapo tele.

Hayo yanafanyika mnamo wakati misuguano ya kisiasa ikitishia hata kuyavuruga mafanikio ambayo yameshapatikana katika mchakato wa kutekeleza makubaliano ya amani.

Rais wa Sudan Kusini Salva KiirPicha: Reuters/T. Negeri

Kiir na Machar washindwa kuelewana kuunda jeshi la pamoja!

Machar na Kiir wameshindwa kuelewana kuhusu vipengee muhimu mathalan, kuunda jeshi la Pamoja litakalovileta pamoja vikosi vya pande tofauti chini ya kamandi moja.

Huku ikiwa imesalia muda wa mwaka mmoja kabla ya uchaguzi kufanyika nchini humo, Sudan Kusini iko katika hatari ya kutumbukia kwenye machafuko tena.

Hayo ni kulingana na tahadhari iliyotolewa mapema mwezi huu na Umoja wa Mataifa.

Familia ya Henry ambayo kwa sasa inaishi kama wakimbizi nchini Uganda ni miongoni mwao.

Henry mwenye umri wa miaka 40, anafanya kazi mbili mjini Juba; kuwsafirisha watu kutumia baiskeli binafsi ili kuipiga jeki kazi yake ya ualimu ambayo hulipwa mshahara wa dola 35,000 za Sudan Kusini, ambayo ni sawa na dola 80 za Marekani. Mshahara huo ni mdogo hivi kwamba anatumia zaidi ya nusu yake kulipa kodi ya nyumba.

Vita vya wenyewe kwa wenyee vya Sudan Kusini vilivyoanza mwaka 2013 viliwalazimisha mamilioni ya watu kuyakimbia makaazi yao.Picha: Reuters/T. Negeri

Taifa tajiri wa mafuta lakini uchumi wake umedorora

Licha ya kuwa taifa lenye utajiri wa mafuta, uchumi wa Sudan Kusini ‘umeshikwa mateka' na ufisadi wa kisiasa. Ndivyo ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa mwezi Septemba ilivyoeleza ikiwatuhumu viongozi serikalini kwa kujilimbikizia mamilioni ya dola ambazo ni fedha za umma kwa masilahi yao wenyewe.

Sudan Kusini yapuuza ripoti ya UN kuhusu ufisadi wa wanasiasa wake

Nchi hiyo imeorodheshwa ya chini kabisa katika faharasa ya nchi fisadi ulimwenguni iliyotolewa na shirika la kupambana na ufisadi Transparency International.

Kwa mujibu wa takwimu za Marekani, asilimia 75 ya jumla ya raia milioni 11 wa Sudan Kusini walihitaji misaada ya kiutu mwaka uliopita.

Katika kila raia watano wa Sudan Kusini, wanne miongoni mwao wanaishi Maisha ya umaskini. Robo tatu ya raia wote wakielezwa kuathiriwa na njaa kali. Hayo ni kulingana na takwimu za Benki ya Dunia ya mwaka 2018.

Je serikali itaweza kuandaa uchaguzi mwaka ujao?

Takwimu mbalimbali ikiwemo ya Umoja wa Mataifa zimeeleza kuwa idadi kubwa ya watu Sudan Kusini walikabiliwa na njaa kali mwaka 2021. Picha: Simon Wohlfahrt/AFP

Baada ya miaka mingi ya misukosuko, ni watu wachache pekee ndio wana matumaini kuwa serikali ya nchi hiyo inayozongwa na ugomvi wa ndani kwa ndani, itaweza kupiga hatua mbele kuelekea tarehe ya uchaguzi mkuu mwaka ujao.

Sudan Kusini yaadhimisha miaka 10 ya uhuru

Boboya James ambaye ni mchambuzi katika taasisi kuhusu Sera za Sosholojia na Utafiti iliyoko Juba, amehoji kwamba ni heri muda wa mkataba wa amani urefushwe kwa mwaka mmoja au miwili ili maafisa wa serikali waweze kujiandaa sawa katika kutekeleza vipengee vilivyosalia vya mkataba wa amani na kuandaa uchaguzi.

Ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, miongoni mwa mambo yale ambayo serikali inapaswa kutekeleza, ni pamoja na kuhakikisha kuna katiba, jeshi lililoungana, mahakama na mchakato wa uchaguzi kuwekwa.

Hadi hayo yatakapotekelezwa, Henry hatarajii kuirudisha familia yake nyumbani Sudan Kusini kutoka Uganda.

(AFPE)