1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchakato wa kumchagua Papa waendelea

Admin.WagnerD13 Machi 2013

Baada ya makadinali wa Kanisa Katoliki hapo jana kukosa kuafikiana kuhusu ni nani atakuwa mkuu wa kanisa hilo, leo mchakato huo unaendelea katika makao makuu ya kanisa hilo, Vatican.

Black smoke rises from the chimney on the roof of the Sistine Chapel in the Vatican City indicating that no decision has been made after the first day of voting for the election of a new pope, March 12, 2013. Roman Catholic Cardinals started a conclave on Tuesday to elect a successor to Pope Benedict, who abdicated last month. REUTERS/Tony Gentile (VATICAN - Tags: RELIGION TPX IMAGES OF THE DAY)
Moshi mweusi ukifukaPicha: Reuters

Makadinali hao wanamuomba Mungu kuwa na maono ya kuweza kumchagua kiongozi wao. Jumla ya makadinali 115 walio na jukumu la kumchagua papa mpya baada ya Benedict wa 16 kujiuzulu mwezi uliopita, leo walihudhuria misa ya asubuhi katika kanisa la Pauline ndani ya makao makuu ya Vatican.

Baada ya hapo wamerejea katika kanisa dogo la Sisitine ili kupiga kura, shughuli ambayo inatarajiwa kuwa na awamu mbili leo asubuhi na nyingine mbili mchana wakitafuta kumchagua kiongozi wa Kanisa Katoliki atakayekuwa na uwezo wa kukabiliana na misururu ya kashfa na mizozo ya ndani kwa ndani inayolikumba Kanisa hilo katika miaka ya hivi karibuni.

Waumini, watalii wasubiri matokeo

Waumini wa kanisa hilo na watalii walianza kufika katika ukumbi wa Vatican mapema asubuhi wakitumai kushuhudia matokeo ya uchaguzi huo na kusubiri kuuona moshi mweupe ukifuka kutoka kanisa hilo la Sisitine.

Makadinali 115 wanaomchagua Papa mpya wa KatolikiPicha: Reuters

Hapo jana usiku, moshi mweusi ulionekana ukifuka kutoka Vatican ishara kwamba makadinali hawajaafikiana kuhusu ni nani atachukuwa wadhifa wa Baba Mtakatifu. Mara baada ya kuafikiana kwa kupata thuluthi mbili ya kura, moshi mweupe utaonekana na kengele za kanisa kuu la Mtakatifu Petro kupigwa.

Hali ilikuwa kinyume na matarajio

Makadinali hao jana walifungiwa katika kanisa la Sisitine kwa siku ya kwanza baada ya ibada na maombi ya kuwatayarisha kwa ajili ya wajibu huo muhimu katika kanisa Katoliki. Jana usiku kura ilipigwa mara moja na kama ilivyotarajiwa na wengi, makadinali hawakuafikiana.

Makadinali wakiwa katika misa maalumPicha: Reuters

Hakuna baraza la makadinali katika nyakati za sasa ambalo limemchagua papa katika siku ya kwanza ya upigaji kura, kwa hivyo matokeo ya hapo jana hayakupokelewa kwa mshangao. Kawaida awamu ya kwanza huchukuliwa kama mchujo wa wanaopigiwa upatu.

Vatican imechukua hatua za tahadhari ili kusiwepo kwa mawasiliano ya aina yoyote kati ya makadinali hao 115 na ulimwengu kuepusha ushawishi wa nani atakayechaguliwa. Hakuna matumizi ya simu, redio, televisheni wala mitandao.

Kashfa za kanisa katoliki

Papa mpya ataubeba mzigo uliomfanya Papa Benedict wa 16 kutangaza mwezi Februari kuwa umemuelemea. Kanisa Katoliki linazongwa na kashfa chungu nzima za udhalilishaji watoto na visa vya kufichuka kwa siri za makao makuu yake ya Vatican zinazodai kuwepo kwa ufisadi na malumbano ya wenyewe kwa wenyewe.

Kiongozi aliyejiuzulu Papa Benedict XVIPicha: Reuters

Aidha linakumbwa na ushindani kutoka makanisa mengine katika udhibiti wa wafuasi hasa barani Ulaya ambayo ni ngome yake. Inakisiwa kuwa kanisa hilo lina waumini bilioni 1.2 kote duniani.

Wanaopigiwa upatu kutangazwa kuwa papa mtakatifu mpya ni Angelo Scola kutoka Italia, Mbrazil Odilo Sherer ambaye akichaguliwa atakuwa papa wa kwanza ambaye hatoki barani Ulaya tangu kuchaguliwa kwa Papa Gregory III yapata miaka 1300 iliyopita.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/dpa
Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW