1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchakato wa kumng'atua Rousseff kuendelea

10 Mei 2016

Mkwamo uliojitokeza jana kuhusu mchakato wa kumwondoa madarakani Rais wa Brazil Dilma Rousseff umepata ufumbuzi, baada ya kaimu Spika wa Bunge kusema leo kuwa amebadilisha uamuzi wake wa awali wa kuufuta mchakato huo

Brasilien Dilma Rousseff und anhänger
Picha: picture-alliance/Photoshot

Mapambano kuhusu hatima ya Rais wa Brazil Dilma Rousseff yalionekana kuchukua mkondo tofauti jana baada ya kaimu spika wa bunge Waldir Maranhao kutangaza kuwa ameibatilisha kura iliyopigwa na wenzake mwezi uliopita iliyounga mkono kuondolewa madarakani rais Rousseff.

Mara moja rais wa baraza la Seneti Renan Calheiros alijitokeza na kusema kuwa ataipuuza hatua ya spika wa bunge Maranhao na kuendelea na mchakato huo kama ilivyopangwa. Aliikosoa hatua ya spika akisema ni “kuichezea demokrasia”. "hakuna uamuzi wa upande mmoja unaoweza kuufuta uamuzi wa pamoja, hasa wakati uamuzi huo ulichukuliwa na kwa pamoja bungeni, kwenye kikao kamili, na isitoshe, na idadi akidhi iliyothibitishwa ya wabunge"

Lakini sasa spika Maranhao amesema leo katika taarifa kuwa ameubadilisha uamuzi wa kuifuta kura hiyo ya wabunge iliyopigwa Aprili na hivyo kuruhusu kuendelea kwa mchakato wa kumvua mdaraka rais Rousseff

Kaimu spika wa bunge la Brazil Waldir MaranhaoPicha: Imago/ZUMA Press

Baraza la Seneti linatarajiwa kupiga kura kesho Jumatano kama litaikubali kesi ya kuondolewa madarakani Rousseff na kumfungulia mashitaka kwa tuhuma za kuvunja sheria za kifedha katika usimamizi wake wa bajeti ya taifa. Ikiwa maseneta watapiga kura ya kuunga mkono mchakato huo, Rousseff atasimamishwa kazi na Makamu wa Rais Michel Temer atachukua usukani hadi kesi dhidi yake itakapofanyika.

Akitangaza uamuzi wake jana spika, Maranhao alisema kura hiyo ilikumbwa na dosari nyingi, na ikiwa ni pamoja na ukiukaji wa sheria, kama vile viongozi wa vyama kuwaambia wanachama namna ya kupiga kura. Ameongeza kuwa kura ya kwanza tayari ilionekana "kumhukumu" Rousseff na kumnyima "haki ya kujitetea kikamilifu"

Rousseff alijibu kwa uangalifu tangazo la Maranhao, akidokeza kuwa haijabainika wazi kikamilifu kinachoendelea kwa sasa. “azma yangu ni kupambana hadi mwisho, na kwamba sasa lazima tuilinde demokrasia, tupigane dhidi ya njama ya mapinduzi, tupigane dhidi ya mchakato mzima usio wa haki ambao umekuwa ni mapinduzi dhidi yangu".

Chini ya masharti ya uamuzi wa Maranhao, bunge lingetakiwa kuwa na vikao vitano kuandaa kura nyingine kuhusu kama liwasilishe katika baraza la Seneti mchakato wa kumvua madaraka Rousseff au la.

Maranhao alichukua uongozi wa bunge baada ya spika wa zamani Eduardo Cunha, ambaye alikuwa mstari wa mbele katika jitihada ya kumvua mdaraka Rousseff, kusimamishwa kazi kuhusiana na tuhuma za rushwa dhidi yake na kuzuia kupatikana haki

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Iddi Ssessanga