Mchakato wa kutafuta amani Syria
27 Mei 2013Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, na wenzake wa Urusi na Ufaransa wanakutana leo mjini Paris ili kupanga mikakati zaidi ya kuandaliwa kwa mkutano wa amani unaonuia kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe Syria ambavyo vimeshachukuwa zaidi ya miaka miwili sasa.
Hata hivyo, mazungumzo yalikwama hapo jana kwa upande wa Upinzani wa Syria mjini Istanbul Uturuki yalipoingia siku ya nne baada ya kukosa kuafikiana kuhusu kushirikisha makundi mengine ya upinzani kwenye meza ya mazungumzo itakayowakilisha upinzani katika mazungumzo ya amani ya Geneva.
Mazungumzo hayo ya kimataifa ambayo yamepewa jina la "Geneva 2" yanakuja baada ya mkutano mwezi Juni mwaka jana ambayo yalibuni mpango wa amani uliokosa uungwaji mkono na kusababisha kujiuzulu kwa Kofi Annan kama mjumbe maalum wa kimataifa kwa Syria.
Mitizamo tofauti kuhusu Syria
Kabla ya mkutano wa leo wa Paris kati ya waasisi wa maandalizi wa mkutano huo wa Geneva, mawaziri 27 wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Brussels, huku umoja huo ukiwa umegawanyika sana kuhusu iwapo uwape waasi wa Syria silaha au la.
Baada ya miezi kadhaa ya vuta nikuvute, suala hilo la silaha linatarajiwa kupewa kipaumbele kwenye mkutano wa leo. Uingereza na Ufaransa zimekuwa zikishurutisha kuendelea kuwekwa vikwazo vya kupigwa marufuku kwa utawala wa Assad kupata silaha, lakini wakati huo huo zikisisitiza kuwa upinzani unahitaji kupewa silaha ili kujihami.
Lakini shirika la kimataifa la kutoa misaada ya kibinadamu la Oxfam limeonya kuwa kuingizwa silaha zaidi nchini Syria kutazidi kuchochea vita hivyo na kutasababisha maafa makubwa.
Upinzani wa Syria unaotaka kumng'oa madarakani Rais Assad umeshindwa kupatana katika kura iliyopigwa leo katika mkutano wa Istanbul wa kupanua ushiriki wa makundi mengine chini ya mwavuli wa muungano wa kitaifa wa upinzani.
Upinzani wagawanyika
Licha ya hayo, mkereketwa na msomi wa nadharia ya Marx, Michel Kilo, amejumuishwa na upinzani na hivyo basi inaamaanisha atawashirikisha wanawake na wanachama wa jamii za kidini walio wachache, suala ambalo wachambuzi wanasema litapunguza ushawishi wa Udugu wa Kiislamu na kuipa Saudi Arabia udhibiti wa muungano huo.
Waziri wa mambo ya nje wa Syria, Walid Moualem, hapo jana alisema upande wa serikali utashiriki katika mazungumzo ya Geneva na kwamba inatoa fursa nzuri ya kupata suluhisho la kisiasa kwa mzozo huo.
Lakini upinzani wa Syria umekuwa ukisisitiza kuwa hautakaribia meza ya mazungumzo hadi Assad akubali kung'atuka madarakani.
Huku hayo yakijiri, mapigano katika mji wa Qusayr yamepamba moto, huku majeshi ya Assad yakisaidiwa na wapiganaji wa kundi la wanamgambo la Hizbullah yakijaribu kuudhibiti mji huo ambayo ni ngome ya waasi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuhusika kwa kundi hilo la Hizbullah katika mzozo wa Syria na kutaka hatua zaidi kufanywa kuzuia kusambaa kwa vita hivyo.
Mwandishi: Caro Robi/afp/ap
Mhariri: Mohammed Khelef