1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchakato wa uchunguzi dhidi ya Trump wafanyika hadharani

13 Novemba 2019

Mchakato wa uchunguzi unaofanywa na baraza la wawakilishi nchini Marekani dhidi ya rais wa nchi hiyo Donald Trump, kwa nia ya kumshitaki bungeni umeanza kusikilizwa hadharani.

US-Präsident Donald Trump
Picha: picture-alliance/abaca/Y. Gripas

Wabunge watawahoji wanadiplomasia wawili walioelezea wasiwasi wao kuwa Rais Donald Trump aliahidi msaada kwa Ukraine iwapo mtoto wa mpinzani wake wa kisiasa Joe Biden atachunguzwa. Biden anawania kuteuliwa na chama chake kuwa mgombea wa kiti cha urais katika uchaguzi wa mwaka 2020.

Chama cha Democratic pia kinaushutumu utawala wa chama cha Republican kuendesha njia mbili za kidiplomasia, yani moja rasmi na nyengine isio rasmi kupitia wakili binafsi wa Trump, Rudy Giuliani, kitu ambacho kiliuweka hatarini usalama wa taifa.

Watu wa kwanza kutoa ushahidi wao hadharani ni William Taylor mwanadiplomasia mkuu wa Marekani nchini Ukraine pamoja na afisa wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani George Kent. Siku ya Ijumaa, Marie Yovanovitch, balozi wa zamani wa Ukraine anatarajiwa kutoa ushahidi wake. Yovanovitch aliondolewa mwaka huu katikanafasi yake hiyo, kwa kukataa kushirikiana na Giuliani.

Chama cha Democratiki kimekuwa mbioni kuharakisha mchakato huo wa uchunguzi unaodhamiriwa kumuondoa rais Donald Trump madarakani, huku kukiwa na madai kwamba huenda wakakamilisha mchakato huo kabla ya mwisho wa mwaka huu.  

Chama cha Republican kinakishutumu chama cha Democratic kumuandama Trump

Rais wa Marekani Donald Trump na makamu wa rais wa zamani wa Marekani Joe Biden

Trump kwa upande wake amesema hapakuwa na aina yoyote ya nipe nikupe kama inavyofahamika na ametoa nakala ya maandishi inayoelezea mawasiliano yake kwa njia ya simu na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

Lakini wakosoaji wa rais huyo wanasema simu hiyo imeonesha kumekuwepo na msukumo wa aina fulani kwa Ukraine na kuzungumzia pia zingatio la Trump kutaka Biden kuchunguzwa, Ijapokuwa hakuna ushahidi wowote wa uhalifu uliofanywa na Biden, ambaye ni Makamu wa rais wa zamani wa Marekani.

Chama cha democratiki ndicho kilichokuwa kinasimamia sera za Ukraine  mwishoni mwa utawala wa rais wa zamani Barrack Obama, na mtoto wa Biden alikuwa na mshahara mkubwa kama mwanachama wa bodi ya kampuni ya Nishati nchini Ukraine.

Lakini suala la iwapo mchakato wa leo ndio utakaokuwa mwanzo wa kuhitimisha uongozi wa rais au kusaidia kudhibiti nafasi ya Trump, ni wazi kwamba muhula wake mgumu umeanza na kufikia mahali ambako hawezi kuudhibiti.

Huku hayo yakiarifiwa chama cha Republican kimekishutumu chama cha Democatiki kwa kujaribu kumuondoa rais wao tangu alipochukua madaraka kwa mara ya kwanza miaka mitatu iliyopita, kupitia uchunguzi wa Robert Muller kuhusu Urusi kuuingilia uchaguzi wa Marekani kwa nia ya kumsaidia Rais Trump katika uchaguzi wa mwaka 2016.

Chanzo: dpa/afp

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW